IQNA

Nakala za Qur'ani zilizochapishwa bila ruhusa zakusanywa Imarati

12:11 - July 08, 2012
Habari ID: 2363313
Idara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Imarati imeanza kukusanya nakala za Qur'ani Tukufu zilizochapishwa bila ya ruhusa ya vyombo husika.
Kituo cha habri cha Khaleej Times kimemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Imarati Bwana Muhamamd Matar al Kaabi akisema kuwa idara yake imegundua nakala za Qur'ani Tukufu zilizochapishwa bila ya ruhusa ya vyombo husika na kusambaza nchini humo.
Uchapishaji na usambazaji wa nakala za Qur'ani Tukufu nchini Imarati hufanyika chini ya usimamizi wa Idara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ili kuhakikisha kwamba nakala hizo hazina makosa ya kichapa.
Al Kaabi amesema pamoja na hayo kumeshuhudiwa nakala za Qur'ani Tukufu ambazo hazikuidhinishwa na Idara ya Wakfu. "Nakala hizo zimeingizwa nchini kinyume cha sheria", amesisitiza al Kaabi.
Ametahadharisha kuwa iwapo itathibitika kwamba shirika lolote la uchapishaji la ndani au nje ya nchi linasambaza nakala za Qur'ani Tukufu zenye makosa ya kichapa basi nakala hizo zitakusanya mara moja na mchapishaji wake atachukuliwa hatua za kisheria. 1047433

captcha