IQNA

Mashindano ya Kitaifa ya Qur'ani Nchini Kyrgyzstan Yafikia Tamati

17:07 - October 31, 2025
Habari ID: 3481438
IQNA – Mashindano ya Tatu ya Kitaifa ya Qur'an nchini Kyrgyzstan yametamatika rasmi kwa hafla maalum iliyofanyika siku ya Jumatano.

Washindi wa mashindano ya wavulana na wasichana walitunukiwa zawadi katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Bishkek, kwa mujibu wa tovuti ya al-Madina.

Fainali za mashindano hayo zilifanyika katika Msikiti Mkuu wa Imam Sarakhsi mjini Bishkek kuanzia Oktoba 27 hadi 29. Mashindano haya yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Kiislamu, Da’wah na Mwongozo ya Saudi Arabia na Mamlaka ya Kiislamu ya Waislamu wa Kyrgyzstan.

Hatua za awali zilianza Oktoba 10, zikiwahusisha washiriki kutoka mikoa saba na miji miwili ya nchi hiyo. Jumla ya washiriki 300 walijiunga katika awamu za mwanzo, ambapo 54 kati yao walifaulu kufikia fainali.

Kwa mujibu wa waandaaji, lengo kuu la mashindano haya ni kuhamasisha usomaji na uhifadhi wa Qur'an Tukufu miongoni mwa wananchi wa Kyrgyzstan.

Kyrgyzstan ni nchi isiyo na pwani, yenye milima mingi, iliyoko Asia ya Kati. Inapakana na Kazakhstan upande wa kaskazini, Uzbekistan upande wa magharibi na kusini-magharibi, Tajikistan upande wa kusini-magharibi, na China upande wa mashariki. Mji mkuu wake ni Bishkek.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa asilimia 80 ya wakazi wa Kyrgyzstan ni Waislamu.

3495204

captcha