IQNA

Vipindi vya televisheni Misri kulenga kutambua vipaji vya Qur’ani

12:55 - November 13, 2025
Habari ID: 3481511
IQNA – Kipindi cha televisheni kiitwacho “Dawlat al Telawah”, ambacho ndicho shindano kubwa zaidi cha vipaji vya usomaji na tartiil ya Qur’ani, kimepangwa kurushwa kupitia vituo vya satelaiti vya Misri.

Mashindano haya ya usomaji na tartiil ya Qur’ani yataanza kutangazwa kuanzia Ijumaa, tarehe 14 Novemba, kupitia vituo vya satelaiti vya Al-Hayat, CBC, Al-Nas, Misr Qur’an Kareem pamoja na jukwaa la kidijitali “Watch It”.

Muda wa matangazo ya kipindi hiki utakuwa saa 3 usiku kila Ijumaa na Jumamosi.

Kipindi cha “Dawlat al Telawah” kimezalishwa na Wizara ya Awqaf ya Misri kwa ushirikiano na Kampuni ya Al-Muttahida Media Services, kwa lengo la kutambua vipaji vya Qur’ani na wasomaji mashuhuri kutoka mikoa mbalimbali ya nchi.

Thamani ya jumla ya zawadi ni pauni milioni 3.5 za Kimasri, ambapo washindi wa kila moja ya makundi mawili ya usomaji na tartiil watapokea pauni milioni 1.

Usomaji wa Qur’ani nzima na washindi hao wawili utarekodiwa na baadaye kurushwa kupitia mtandao wa “Egypt Qur’an Karim”. Aidha, washindi hao wataongoza swala za jamaa katika Msikiti wa Imam Hussein (AS) mjini Cairo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ujao.

Hatua za awali za mashindano haya zimepokelewa kwa shauku kubwa, ambapo zaidi ya washiriki 14,000 kutoka mikoa mbalimbali walijitokeza kushiriki.

Uhakiki wa washiriki umefanyika kwa hatua kadhaa, na watu 32 wamechaguliwa kushindana katika hatua za mwisho chini ya usimamizi wa kamati maalum ya kielimu kutoka Wizara ya Awqaf, ikiongozwa na Waziri wa Awqaf Osama Al-Azhari.

Jopo la majaji linajumuisha wanazuoni wataalamu wa Qur'ani kutoka Misri na sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu.

3495381

captcha