
Katika makala ya maoni, Malazadeh alinukuu aya ya Qur'ani isemayo: “Na tumekufanyeni mataifa na makabila ili mjuane” (Al-Hujurat 49:13), akieleza kuwa ni “tamko la kimaadili kuhusu utofauti wa kibinadamu.”
Alisema aya hiyo haipaswi kutazamwa kama “sababu ya kujitenga au kuweka daraja za kitamaduni,” bali kama “msingi wa kutambuana na kukubali wengine kwa moyo wa udugu.”
Kwa mujibu wake, katika muktadha wa utandawazi, aya hii inatoa ujumbe wa pande mbili. “Kwanza,” alisema, “muungano wa kimataifa unapaswa kujengwa juu ya heshima ya pande zote na kutambua tofauti zilizopo. Utandawazi wa kweli ni ule unaounda mazingira ya tamaduni kujifunza, kufahamiana, na kunufaika kwa pamoja.”
Aliongeza kuwa “mchakato wowote wa utandawazi unaobomoa utambulisho wa watu au kuwadhalilisha hauendani na roho ya aya hii.”
Malazadeh alibainisha kuwa Qur'ani “haikatai utofauti wala haikubali kila tofauti bila tafakuri, bali inaweka misingi ya uhusiano wa kitamaduni , kutambuana, heshima ya kibinadamu, na kukataa dhulma.”
Alisema kuwa ili mafundisho ya Qur'ani yaweze kuwa muundo wa mazungumzo ya kitamaduni, “dhana hizi kuu lazima zigeuzwe kuwa mifumo ya vitendo.”
Alifafanua kuwa heshima ya kibinadamu inamaanisha “usawa wa kisheria na kusikilizana kwa kuheshimiana,” na akanukuu kanuni ya Qur'ani isemayo: “Hakuna kulazimisha katika dini” (Al-Baqarah 2:256) kama “dhamana ya uhuru wa imani na kukataa kulazimisha kitamaduni.”
Pia alitaja ‘mashauriano’ (shura) na ‘haki’ (qist) kama “viwango vya maamuzi ya pamoja na ya haki.”
Malazadeh alipendekeza kuwa utekelezaji wa misingi hii unahitaji mwenendo wa kimaadili ; kama vile kuepuka lugha ya dharau, kudumisha nia njema, na kuonyesha unyenyekevu wa kielimu, pamoja na hatua za kitaasisi na kimfumo kama “majukwaa ya mazungumzo, elimu ya kitamaduni, sera dhidi ya ubaguzi, usikilizaji wa kina, na miradi ya ushirikiano.”
Alisisitiza kuwa “mtazamo wa kina na wa kimaelezo katika maandiko ya dini unaozuia matumizi mabaya ya Qur'ani kwa ajili ya madaraka au maslahi binafsi ni muhimu kwa kudumisha mazungumzo ya kweli.”
Kupitia mtazamo huo, alisema, “mafundisho ya Qur'ani yanaweza kutoa muundo thabiti wa maadili kwa mawasiliano ya kitamaduni na nyenzo halisi za ushirikiano wa amani na wa kujenga, sambamba na mbinu za kijamii na kisheria za kisasa.”
/3495214