IQNA

Maonyesho ya 20 ya Kimataifa ya Qur'ani kufunguliwa Tehran

11:18 - July 14, 2012
Habari ID: 2367333
Maonyesho ya 20 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran yatafunguliwa rasmi Julai 15 katika sherehe itakayohudhuriwa na Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Haya ni kwa mujibu wa Alireza Taqipour ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya utendaji katika maonyesho hayo. Katika mahojiano na IQNA, amesema maonyesho hayo yatafanyika katika Ukumbi Mkubwa wa Sala wa Imam Khomeini SA baada ya sala za Magharibi na Ishaa.
Amesema maonyesho hayo yatakuwa wazi kila siku kuanzia saa 11 jioni hadi saa sita usiku katika siku za kazi na saa nane mchana hadi saa sita usiku katika siku za wikendi.
Ameongeza kuwa maonyesho ya mwaka huu pia yatajumuisha washiriki kutoka nchi kama vile ndia, Pakistan, Bahrain, Albania, Uturuki, Thailand, Iraq, Myanmar, Syria, Afghanistan, Bosnia na Herzegovina na Sri Lanka.
Taqipour ameendelea kusema kuwa maonyesho hayo yatakuwa na vitengo 40 vyote vyenye lengo la kueneza na kustawisha mafundisho ya Qur'ani Tukufu na vile vile kuwaelimisha watu kuhusu Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa katika eneo. Aidha amesema maonyesho ya mwaka huu yatazingatia zaidi suala la watoto na vijana ili kuwaelimisha zaidi na vile vile kuwawezesha kuisoma na kuihifadhi Qur'ani.
Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran hufanyika kila mwaka na kawaida huanza siku chache kabla ya kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuendelea hadi siku chache kabla ya kumalizika mwezi huo mtukufu.
1051663
captcha