IQNA

Shakhsia mashuhuri waliosilimu waarifishwa katika maonyesho ya Qur'ani ya Tehran

15:22 - July 18, 2012
Habari ID: 2371763
Kibanda maalumu cha kuwaarifisha watu na shakhisa mashuhuri waliosilimu na kuikubali dini tukufu ya Kiislamu duniani kimeanzishwa kwa mara ya kwanza katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran.
Kibanda hicho kinawasilisha historia fupi ya watu hao mashuhuri duniani ambao wamesilimu na vilevile kukubali madhehebu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) yaani Ushia.
Kitengo hicho kimesema kuwa kimepokea wageni wengi wanaoyatembelea maonyesho hayo kwa ajili ya kujua maisha na masuala yaliyowavutia Waislamu hao wapya na kuwafanya waukubali Uislamu.
Franck Bilal Ribery mchezaji mashuhuri wa mpira wa miguu anayechezea klabu ya Ujerumani ya Beyern Munich katika ligi ya Bundesliga na ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Muhammad Ali Clay bondia mashuhuri wa Marekani na Edoardo Agnelli, mwana wa tajiri mmoja mashuhuri wa Italia ni miongoni mwa watu waliosilimu ambao visa vyao vya kusilimu vimewavutia wengi wanaotembelea maonyesho hayo.
Kibanda hicho cha watu waliosilimu pia kinawaarifisha wahubiri mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu wakiwemo Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhsin Qaraati, Sayyid Hassan Nasrullah, Hujjatul Islam Mazari na Ayatullah Ali Sistani ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kueneza Uislamu halisi duniani.
Kibanda hicho pia kinawashirikisha watu waliosilimu katika vikao vya kuwafahamisha wageni wanaokitembelea sababu za kusilimu kwao.
Maonyesho ya 20 ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya mjini Tehran ambayo yalianza siku ya Jumatatu tarehe 16 Julai yataendelea kwa muda wa karibu mwezi mmoja na yamepangwa kumalizika tarehe 14 Agosti. 1055947
captcha