IQNA

Usitishwaji mapigano Ghaza ni ushindi kwa Wapalestina

11:02 - November 23, 2012
Habari ID: 2453145
Duru mbalimbali za kidiplomasia na kisiasa zinaamini kuwa, usitishwaji mapigano kati ya utawala haramu wa Israel na wanamapambano wa Palestina ni ushindi mkubwa kwa mrengo wa makundi ya Hamas na Jihadul Islami na kwamba utawala ghasibu umepata pigo kubwa.
Vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo kanali mashuhuri kama vile CNN, BBC, PressTV na Aljazeera zimetoa tathmini kwamba Israel mbali na kuwa ndiyo iliyoanzisha mapigano, ilishindwa kufikia malengo yake sambamba na kuogopa kupeleka majeshi ya ardhini katika Ukanda wa Ghaza kwa hofu ya kufikwa na maafa makubwa. Gazeti la New York Times limeandika kuwa, hatua ya Israel ya kuwaua watoto wadogo na wanawake imeonyesha kufilisika kimawazo utawala huo haramu.

Baada ya siku nane za vita vya umwagaji damu katika Ukanda wa Ghaza hatimaye utawala wa Kizayuni wa Israel umesalimu amri mbele ya irada ya muqawama na kuukubali bila ya masharti yoyote mpango wa usitishaji vita ambao ulianza kutekelezwa majira ya saa tatu usiku hapo jana. Miongoni mwa vipengele vya makubaliano hayo ni kusimamishwa mashambulio ya anga, ardhini na baharini ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza, kusitishwa mashambulio ya wanamuqawama wa Palestina dhidi ya Israel na kufunguliwa vivuko vinavyoishia Ghaza masaa 24 baada ya kuanza kutekelezwa usitishaji vita huo ili kuruhusu uingiaji na utokaji wa watu pamoja na upitishaji wa bidhaa. Kukomeshwa mauaji ya kigaidi ya shakhsia wa Kipalestina yanayofanywa na utawala haramu wa Israel ni kipengele kingine kilichomo kwenye makubaliano hayo.

Usitishaji huo wa vita vya kidhalimu dhidi ya Ghaza umefikiwa kutokana na harakati za kidiplomasia za usuluhishi uliofanywa na Misri baina ya pande mbili za Hamas na utawala wa Kizayuni. Kiasi kwamba hata wakati wa kuanza kutekelezwa usitishaji mapigano ulitangazwa rasmi na Waziri mwenyewe wa Mambo ya Nje ya Misri katika mkutano mbele ya waandishi wa habari. Takriban sambamba na kutangazwa mpango huo wa usitishaji vita Shaul Mofaz, Waziri wa zamani wa vita wa utawala haramu wa Israel alikiri kwamba Hamas ndio iliyoibuka mshindi, na Israel ni mshindwa mkubwa katika vita vya Ghaza.

Na huo ndio ukweli wa mambo. Kwani utawala wa Kizayuni ulianzisha mashambulio dhidi ya Ukanda wa hGaza siku ya Jumatano ya tarehe 17 mwezi huu wa Novemba ukidhani kwamba utaweza kufikia haraka malengo uliyokusudia na kuiweka kwenye mashinikizo harakati ya muqawama ya Hamas. Utawala ghasibu wa Israel ulikuwa na mategemeo na matarajio makubwa kwa mfumo wake wa kujihami na makombora unaojulikana kama Kuba la Chuma kwa kimombo 'Iron Dome' na hasa ikizingatiwa pia kwamba kama ilivyo ada na desturi ya kila mara, serikali ya Marekani iliunga mkono kikamilifu jinai mpya za mashambulio ya kinyama yaliyoanzishwa na utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Hata hivyo radiamali ya Hamas kwa mashambulio ya utawala wa Kizayuni katika siku tatu tu za kwanza za vita ya kufyatua makombora kuelekea Telv Aviv na kufika hata kwenye miji ya mbali zaidi ya mji mkuu huo wa Israel na kushindwa mfumo wa Kuba la Chuma kutungua mengi ya makombora hayo ilidhihirisha wazi kuwa mara hii utawala wa Kizayuni umekwenda mchomo kimahesabu. Katika duru hii mpya ya mashambulio yake dhidi ya Ghaza, utawala wa Kizayuni ulikuwa ukidhani kwamba hali ya sasa ni sawa na ya miaka minne iliyopita wakati ulipofanya mashambulio ya kinyama ya siku 22 dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo, ilhali hali ya Hamas na muqawama kwa ujumla hivi sasa inatafautiana sana na ya wakati ule. Katika muda wa siku nne tu za kwanza za mashambulio ya hivi majuzi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza zaidi ya makombora mia nane ya wanamuqawama wa Palestina yalielekezwa Tel Aviv na katika miji mingine ya kandokando yake ambapo mfumo wa kujihami wa Kuba la Chuma uliweza kutungua makombora 245 tu kati ya hayo, hali iliyodhihirisha nguvu na uwezo wa kijeshi wa muqawama wa Palestina ambao Israel haikuweza hata kuufikiria.

Ukweli ni kwamba makombora yaliyotua ndani ya Tel Aviv yaliushtua mno na kuufadhaisha utawala haramu wa Israel. Na joto la hali hiyo ya kiwewe na fadhaa likawa linazidi kupanda ndani ya kipindi cha siku nane za vita kadiri wanamuqawama wa Palestina walivyoendelea kujibu mapigo kwa mashambulio ya anga na baharini ya utawala wa Kizayuni kiasi kwamba kutokana na mhemko wa wahka na kiwewe kilioupata, utawala huo ulichukua hatua haraka ya kuwataka waitifaki wake wafanye jitihada za kufanikisha usitishaji vita.

Fahmi Huwaydi, mwandishi maarufu wa Kimisri anasema kuhusiana na vita vya karibuni vya Ghaza kwamba hakuna aliyetarajia kuwa kutokana na jinsi Israel ilivyoanzisha mashambulio kwa vishindo na makeke ingekanganyikiwa haraka na kuwataka viongozi wa Misri, Ufaransa na hata Uturuki wafikirie njia ya kusimamisha vita. Pamoja na hayo swali linaloulizwa hivi sasa ni je, utawala wa Kizayuni utaheshimu makubaliano hayo ya usitishaji mapigano uliyofikia na Hamas?

Rekodi ya huko nyuma ya Israel inaonyesha kuwa Wazayuni si wenye kuheshimu makubaliano na wala si watekelezaji wa ahadi wanazotoa kwa Waarabu hasa Wapalestina. Lakini nukta iliyo dhahiri ni kwamba muqawama wa Palestina hauko tena katika hali ya huko nyuma ya mmea mchanga unaojikakamua bali sasa ni mti imara uliokua na kukomaa kiasi kwamba kwa kuonyesha sehemu moja tu ya nguvu na uwezo wake umeuendesha mchakamchaka utawala wa Kizayuni na kuulazimisha ukubali masharti ya usitishaji vita yaliyotolewa na Hamas.
1142537
captcha