IQNA

Rais Ahmadinejad: Waislamu waungane kuuangamiza Uzayuni

21:32 - January 27, 2013
Habari ID: 2487250
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu wa madhehebu na mataifa yote duniani kuungana juu ya misingi na malengo makuu ya Uislamu na kusisitiza kwamba kupambana hadi kuuangamiza Uzayuni inabidi liwe ni moja ya malengo hayo makuu ya Waislamu.
Ameongeza kuwa wakati utawala wa Kizayuni ambao ni pandikizi, katili, fasidi na usio na ustaarabu unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuwakandamiza, Waislamu hatupaswi kukaa kimya na kuangalia kwa macho tu mambo hayo.
Pia amesisitiza kuwa, Waislamu wanapaswa kuungana dhidi ya madola ya kishetani na kibeberu duniani na kuongeza kuwa, tawhidi, uadilifu na mapenzi kwa wanaadamu wote ni miongoni mwa malengo makuu ya kupigania umoja kati ya mataifa ya Kiislamu.
Rais Ahmadinejad amesema hayo leo Jumapili kwenye Mkutano wa 26 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaoendelea hapa mjini Tehran.
Mkutano huo unawajumuisha wanavyuoni, wasomi na shakhsia mbalimbali wa Kisuni na Kishia kutoka nchi 102 ulimwenguni. Kongamano hilo la kila mwaka hufanyika kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja inayoanza tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Rabiul Awwal. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal.

Kwa msingi huo, Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.
1178614
captcha