Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Alkhamisi mjini Tehran alipooana na makamanda, maafisa na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika hotuba yake amekutaja kuendelea kushuhudiwa mashinikizo na vitisho vya kila nui vya miaka 34 sasa vya Marekani dhidi ya Iran na wakati huo huo viongozi wa nchi hiyo kudai kuwa wako tayari kwa ajili ya mazungumzo na Iran kuwa ni dalili ya kwamba viongozi wa Marekani hawana nia njema na huku akiashiria kuwa macho na kutotishika taifa la Iran katika kukabiliana na harakati za kijanja na kidanganyifu za Wamarekani amesisitiza kuwa: Taifa azizi la Iran lenye tabasuri na muono mpana na lililopambika kwa sifa ya istikama, litashiriki kwenye maandamano ya Bahman 22 (Jumapili Februari 10, 2013 zitakapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) kwa umoja na kwa nguvu kubwa na kwa harakati yake hiyo ya kitaifa na kimapinduzi taifa la Iran litatoa pigo jingine kubwa kwa adui mwenye nia ya kuwafanya wananchi wa Iran wawe mbali na Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Mkutano huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya tangazo la kihistoria la utiifu wa majimui ya makamanda wa Jeshi la Anga la Iran kwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) yaani Bahman 19, 1357 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Februari 8, 1979 Milaadia).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria tofauti kubwa iliyopo baina na nafasi liliyo nayo leo hii taifa la Iran na ile liliyokuwa nayo miaka 34 iliyopita na kuongeza kuwa: Katika kipindi hiki cha miongo mitatu iliyopita, wananchi wa Iran wameyafundisha mataifa mengine ya dunia kuwa inawezekana bali inabidi kusimama kidete kukabiliana na uistikbari wa mabeberu na limeendelea na njia na harakati yake hiyo huru kwa ufakhari na nguvu kubwa kwa msaada na kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja siku za Alfajiri Kumi (siku za maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 ya nchini Iran) kuwa ni fursa nzuri ya kuweza kutathmini harakati ya miaka 34 iliyopita ya Jamhuri ya Kiislamu na ya taifa la Iran katika nyuga na chanjaa tofauti na kuongeza kuwa: Tathmini hiyo itatuonesha ni vipi tuichague njia ya mustakbali bora na tuendelee nayo vipi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia njama mbali mbali za maadui ikiwa ni pamoja na kufanya mapinduzi ya kijeshi, kufanya uchokozi wa kijeshi, kumuunga mkono kwa kila namna adui mshambuliaji, upinzani wa kikorofi na mkali, upinzani laini na wa chini kwa chini, mashinikizo makubwa na vituko vya kila aina vya kambi khabithi ya vyombo vya habari pamoja na mashinikizo makali yanayoongezeka siku baada ya siku na kusisitiza kuwa: Maadui hao wametumia kila fursa waliyoipata kwa shabaha ya kulivunja moyo na kulikatisha tamaa taifa la Iran ili kulifanya taifa hili liuchukie Uislamu na liwe na mtazamo mbaya kuhusu Jamhuri ya Kiislamu na hatimaye kulitoa katika medani taifa hili la kimapinduzi lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na baraka Zake, wananchi wa Iran wamezidi kuwa na hamasa, wako imara na ni waaminifu na waamilifu zaidi.
Vile vile ameashiria matamshi ya baadhi ya viongozi wa Marekani wanaosisitizia kushadidishwa vikwazo ili kuwafanya wananchi wa Iran wapambane na mfumo wao wa utawala yaani Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Taifa la Iran siku zote na hususan katika maandamano ya Bahman 22 kila mwaka, hutoa majibu kwa matamshi hayo (ya viongozi wa Marekani) na mwaka huu pia watafanya vivyo hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja muono wa mbali, tabasuri na kuwa macho kuwa ndiyo siri ya mafanikio ya taifa hili katika kukabiliana na mabeberu na kuongeza kuwa: Wananchi kwa kujipamba kwa sifa ya kuwa macho na kuwa na muono wa mbali kitaifa, wanazijua vizuri njama za Wamarekani na Wazayuni katika harakati zao zote na kwamba wananchi wa Iran hawafanyi kosa katika matendo na misimamo yao na uhakika huo ni bahati nzuri na adhimu kwa taifa hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia jinsi Marekani inavyokariri mara kwa mara madai yake kwamba iko tayari kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Iran matamshi ambayo hivi karibuni pia yamekaririwa tena na viongozi wa Marekani na kuongeza kuwa: Tab'an matamshi ya viongozi hao hayana mapya kwani wamekuwa wakiyatoa na kuyakariri katika nyakati tofauti na mara zote taifa la Iran linayapima matamshi hayo ya viongozi wa Marekani na vitendo vyao viongozi hao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matamshi ya Wamarekani wanaodai kuwa mpira hivi sasa uko kwenye uwanja wa Iran na kusema: Mpira uko kwenye uwanja wenu wenyewe. Kwani ni nyinyi ndio mnaopaswa kubeba majukumu ya hali iliyopo. Kwani kudai tu kuwa mko tayari kwa mazungumzo kunatosha wakati mnashadidisha vitisho na mashinikizo dhidi ya taifa la Iran?
Ameongeza kuwa: Mazungumzo hufanyika kwa ajili ya kuonesha nia njema. Lakini nyinyi mnafanya makumi ya mambo ya kuonesha hamna nia njema hata kidogo halafu mnakuja na madai kuwa mnataka mazungumzo. Hivi kwa hali hii taifa la Iran linaweza kweli kuamini kuwa mna nia njema?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia chanzo na sababu ya Wamarekani kupendekeza kufanyika mazungumzo hivi sasa na kusema kuwa: Tab'an sisi tunawaelewa Wamarekani wanaposema kuwa wana haja na mazungumzo. Kwani siasa za Mashariki ya Kati za Wamarekani zimefeli na hivi sasa wanahitajia karata ya turufu kwa ajili ya kuondoa kufeli kwao huko.
Amesema, kuipeleka Jamhuri ya Kiislamu, ya kimapinduzi na ya wananchi kwenye meza ya mazungumzo ndiyo karata ya turufu inayohitajiwa na Marekani hivi sasa.
Ameongeza kuwa: Wanataka kuuambia ulimwengu mzima kuwa wana nia njema, lakini mtu haioni hiyo nia yao njema.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mapendekezo ya Marekani ya miaka minne iliyopita ya kutaka kuwa na mazungumzo na Iran na kuongeza kuwa: Tangu wakati huo tulisisitiza kuwa sisi hatutabiri wala hatuhukumu chochote kuhusu pendekezo hilo bali tunasubiri vitendo kutoka kwao Wamarekani lakini katika kipindi hiki cha miaka minne iliyopita hatukuona chochote kutoka kwa Wamarekani zaidi ya njama, kuwasaidia wafanya fitna pamoja na kuwaunga mkono magaidi waliowaua kigaidi wasomi na wanasayansi wa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Nyinyi kama mnavyodai wenyewe, mnaweka vikwazo vya kulemaza ili kulifanya kilema taifa la Iran. Sasa huku ni kuonesha nia njema au nia mbaya?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amengeza kuwa: Mazungumzo yanakuwa na maana pale pande mbili zinapoonesha nia nzuri na pande mbili hizo kufanya mazungumzo katika mazingira ya kiuadilifu yasiyo na kuchezana shere na ni kwa sababu hii ndio maana tukasema kuwa "mazungumzo kwa ajili ya mazungumzo," "mazungumzo kwa sura ya kijanjajanja" na kutoa pendekezo la mazungumzo kwa ajili ya kuonesha ubabe duniani; kwa kweli ni hila za kidanganyifu na si mazungumzo kwa maana ya mazungumzo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Mimi si mwanadiplomasia, mimi ni mwanamapinduzi na ni kwa sababu hiyo ndio maana sina masuala ya kuzunguka zunguka katika maneno yangu, bali ninasema waziwazi ninachokikusudia, ninasema lililo la kweli na bila ya kumuogopa mtu: Pendekezo la mazungumzo linakuwa na maana pate tu upande husika unapoonesha nia nzuri.
Vile vile amewatanabahisha Wamarekani akiwaambia: Nyinyi mnawaelekezea silaha wananchi wa Iran na kuwaambia imma njooni tuzungumze au tutakupigeni risasi! Lakini tambueni kuwa mazungumzo hayakai zizi moja na vitisho na kamwe taifa la Iran haliwezi kutishwa na vitisho vyenu.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewalaumu wale watu ambao wana fikra finyu na wale wenye nia zao maalumu binafsi ambao wanafurahia pendekezo la mazungumzo lililotolewa na Marekani na kuongeza kuwa: Kufanya mazungumzo na Marekani hakuwezi kutatua jambo lolote lile kwani katika kipindi chote hiki cha miaka 60 iliyopita, Marekani haijawahi kuheshimu wala kutekeleza ahadi yake hata moja.
Kuandaa na kuendesha mapinduzi ya Mordad 28 (Agosti 19, 1953) yaliyoipindua serikali ya Dk Mosadeq nchini Iran tena katika hali ambayo serikali hiyo ilikuwa imewaamini na kuwatumainia Wamarekani na kitendo cha Wamarekani cha kuendelea kuuunga mkono mtawalia utawala dhalimu na wa kidikteta wa Kipahlavi nchini Iran ni mifano miwili ambayo Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameitumia kubainisha vitendo viovu vya Wamarekani dhidi ya Wairani.
Ameongeza kuwa: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, kuna wakati baadhi ya viongozi nchini Iran waliwahi kuwa na matumaini na Wamarekani na wakawaamini, lakini ni wakati huo ndipo Marekani ilipotangaza kuwa Iran ni sehemu ya mhimili wa shari na hivyo kuonyesha dharau kubwa kwa taifa la Iran.
Akitoa muhtasari wa sehemu hiyo ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa kuzingatia tajiriba na uzoefu wa huko nyuma tunasisitiza kuwa mazungumzo na mashinikizo ni vitu viwili tofauti ambavyo kila kimoja kinakwenda upande wake na kwamba wananchi wa taifa la Iran hawawezi kukubali kufanya mazungumzo na mtu ambaye anawashinikiza na kuwatishatisha.
Ameongeza kuwa: Kila mtu anayetaka kuuona ubeberu wa Marekani unarejea tena nchini Iran na ambaye anastahabu radhi za Wamarekani kuliko manufaa na maslahi ya taifa na kufumbia macho maendeleo ya nchi na uhuru wa taifa basi ajue kuwa ghadhabu za taifa zitamuangukia na hata mimi pia kama nitakwenda kinyume na matakwa hayo ya umma basi hasira na malalamiko ya wananchi yatanikumba.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, taifa la Iran ni la watu wapole na wanaopenda amani na ametoa mfano wa jambo hilo kwa kusema kuwa: Sisi tumekuwa tukifanya mazungumzo na nchi yoyote ile isiyoifanyia njama wala uadui Iran na tumekuwa na mawasiliano mazuri na nchi hizo kwani tunajua kuwa jambo hilo lina manufaa kwa taifa letu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, harakati adhimu ya wananchi wa Iran ni harakati ya kudhamini manufaa ya Iran, manufaa ya umma wa Kiislamu na manufaa ya jamii nzima ya mwanadamu na kuongeza kuwa: Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, taifa hili litaufikisha umma kwa Kiislamu kwenye kilele cha fakhari na mafanikio.
Vile vile amekutaja kulindwa umoja, mshikamano na muono wa mbali kuwa ni jambo litakaloandaa uwanja wa kuendelea kushuhudiwa heshima na maendeleo ya taifa na huku akikosoa baadhi ya tabia mbaya zilizooneshwa hivi karibuni na baadhi ya watu nchini amesema kuwa: Viongozi nchini wanapaswa kulinda maslahi ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kuwa, katika siku za usoni atazungumza na wananchi kuhusu tabia hiyo mbaya iliyoonesha hivi karibuni na baadhi ya watu nchini na kuongeza kuwa: Viongozi wanapaswa kuweka kando tabia hiyo mbaya iliyoonekana katika baadhi ya mambo na nyuga, na washikamane na wawe kitu kimoja kama walivyo wananchi na watie nia ya kuwa na lugha na kauli moja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kuwa, kutengenezwa ndege za kivita na ndege nyingine za kila namna pamoja na aina kwa aina ya zana na vifaa vya kisasa ndani ya Jeshi la Anga la Iran; ni ushahidi kuwa ustawi wa vipaji, mapenzi na ubunifu umeenea katika kila kona ya Iran ikiwa ni pamoja na ndani ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Kwa hakika mumeweza kuzibatilisha propaganda za mabeberu wanaojaribu kuonesha kuwa mataifa ya dunia hayawezi kujisimamia na kujiendeshea mambo yao bila ya msaada wa madola ya kibeberu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Brigedia Jenerali Shah Safi, Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Bahman 19 (Februari 7) siku ya kukumbuka tukio la kihistoria la Jeshi la Anga la Iran la kutangaza utiifu wake kwa Imam Khomeini (quddisa sirruh), (Jambo ambalo lilisaidia sana kupatikana kwa haraka ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) ametoa ripoti fupi kuhusu uwezo wa ndani na maendeleo mbali mbali yaliyopatikana ndani ya Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
1185018