IQNA

Wafungwa wa Guantanamo wagoma kula wakipinga kuvunjiwa heshima Qur'ani

10:34 - March 12, 2013
Habari ID: 2510118
Wafungwa wanaoshikiliwa katika jela ya kutisha ya Marekani huko Guantanamo nchini Cuba wameanza mgomo wa kula wakipinga kitendo cha askari wa Marekani cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu.
Mawakili wa zaidi ya wafungwa 10 wa jela hiyo walitangaza jana kuwa mgomo huo unafanyika kupinga upekuzi mpya unayofanywa na askari wa Marekani dhidi ya wafungwa hao ikiwa ni pamoja na kukivunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani.
Wakili wa raia wa Yemen Qalib al Baihani anayeshikiliwa huko Guantanamo amesema kuwa mteja wake pamoja na wafungwa wengine kadhaa wamesema kuwa wenzao wote wanaoshikiliwa katika kambi nambari sita wamo katika mgomo wa kula.
Mawakili wa wafungwa hao wanasema wamemwandikia barua kamanda wa kambi ya Guantanamo wakimpasha habari ya hali mbaya ya wafungwa hao. Wamesema kuwa wamemweleza pia kuhusu vitendo vya askari magereza wa Marekani vya kukivunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani. 1203123
captcha