IQNA

Inna Lillah wa Inna Ilahyi Rajioun

Zaghloul El-Naggar, Gwiji wa Elimu ya Miujiza ya Kisayansi katika Qur’ani, Afariki Dunia Akiwa na Miaka 92

14:34 - November 10, 2025
Habari ID: 3481498
IQNA – Mwanasayansi na msomi wa Kiislamu kutoka Misri, Dkt. Zaghloul Ragheb Mohammed El-Naggar, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 92, kwa mujibu wa taarifa ya familia.

El-Naggar alifariki Jumapili katika mji mkuu wa Jordan, Amman, na kuzikwa Jumatatu baada ya swala ya jeneza katika Msikiti wa Abu Aisha, na maziko yamefanyika katika makaburi ya Umm Al-Qutain.

Alizaliwa tarehe 17 Novemba 1933 katika kijiji cha Mashal, mkoa wa Gharbia, nchini Misri. Alihitimu kwa heshima kutoka Kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Cairo mwaka 1955, na baadaye akapata shahada ya uzamivu (PhD) katika jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Wales, Uingereza mwaka 1963. Aliteuliwa kuwa profesa kamili mwaka 1972.

Katika maisha yake ya kitaaluma, El-Naggar alifundisha na kushika nyadhifa mbalimbali katika taasisi za elimu ndani ya Misri na ulimwengu wa Kiarabu, zikiwemo Chuo Kikuu cha Mfalme Fahd cha Petroli na Madini nchini Saudi Arabia, na Chuo Kikuu cha Qatar. Alikuwa pia mshiriki hai katika mashirika ya kielimu ya kimataifa.

Alijipatia umaarufu kwa kazi zake kuhusu kile alichokiita “miujiza ya kisayansi” ndani ya Qur’ani na Sunnah. Alichapisha zaidi ya makala 150 na vitabu 45, na alishiriki katika vipindi maarufu vya vyombo vya habari vilivyolenga kuangazia uhusiano kati ya imani na sayansi.

Katika maisha yake marefu ya kitaaluma, alipokea tuzo na heshima nyingi, ikiwemo Medali ya Dhahabu ya Sayansi, Fasihi na Sanaa kutoka Jamhuri ya Sudan mwaka 2005.

Kifo chake kimezua salamu za rambirambi kwa wingi katika mitandao ya kijamii, ishara ya athari yake pana katika ulimwengu wa Kiislamu.

3495339

captcha