IQNA

Maafisa Wahimiza Ushiriki wa Wadau Wote wa Qur’ani Katika Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tehran

14:29 - November 10, 2025
Habari ID: 3481497
IQNA – Naibu wa Qur’ani na Etrat katika Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuandaliwa kwa Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu mjini Tehran, kwa ushiriki wa wadau wote wa Qur’ani na Etrat.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika Jumapili mjini Tehran kwa lengo la kunufaika na maoni ya wanazuoni na viongozi wa maonesho ya miaka iliyopita, Hujjatul-Islam Hamidreza Arbab Soleimani alieleza kuwa maonesho haya ni alama ya umoja wa jamii ya Qur’ani ya Iran.

Akitaja nafasi maalum ya Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani ya Tehran, alisema kuwa ni miongoni mwa matukio ya kiutamaduni yenye thamani kubwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hali ya sasa, dunia inakabiliwa na misukosuko mitatu mikuu: kisiasa, kimaadili, na kiuchum, na mizizi ya yote iko katika mgogoro wa maadili. Alisema kuwa roho ya kupenda dunia na anasa imeenea katika jamii za kibinadamu, jambo ambalo limezidisha matatizo ya kimataifa.

"Utamaduni wa kupenda dunia na ubinafsi umeathiri jamii, na hali hii imechochea migogoro mingine. Tiba ya maradhi haya ni kufahamu Qur’ani Tukufu na kutekeleza amri zake," alisisitiza.

Aliendelea kwa kunukuu Qur’ani Tukufu, akisema: Mwenyezi Mungu asema katika Surah Yunus, Aya ya 57: “Enyi watu! Hakika yamekufikieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na tiba ya yaliyomo ndani ya nyoyo.”

Kwa hivyo, alihitimisha kwa kusema kuwa ikiwa dunia ya leo inataka ustawi wa kweli, hakuna njia nyingine ila kuishi kwa mujibu wa Qur’ani.

Akieleza kuwa Maonesho ya Qur’ani ni jukwaa la kuwasilisha maarifa na mafanikio ya Qur’ani, alisema tukio hilo ni kama safari pana ya elimu ya kimungu, ambapo wanaharakati wa Qur’ani nchini wanaweza kushirikiana uzoefu na ubunifu wao.

"Tunatumaini kuwa vikwazo vya kuandaa toleo la 33 la maonesho haya vitaondolewa, ili tuweze kushuhudia tukio lenye heshima linalostahiki hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu," aliongeza.

Hujjatul-Islam Arbab Soleimani pia alieleza kuwa hadi sasa wamefanya takriban mikutano minane ya mashauriano katika Kituo cha Juu cha Qur’ani, wakinufaika na maoni ya wataalamu na wasimamizi wa Qur’ani kuhusu maandalizi ya maonesho.

"Katika hatua mpya, tunapanga pia kutumia maoni ya wataalamu na wasimamizi waliowahi kusimamia maonesho ya Qur’ani katika miaka iliyopita, ili kunufaika na uzoefu wao wa thamani kwa hatua zijazo," alisema.

Ali Reza Moaf, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, pia alizungumza katika kikao hicho, akisema kuwa Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani ni tukio kubwa na baraka ya mfumo wa Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoasisiwa kwa mtazamo wa kimkakati wa Imam Khomeini (RA) na Kiongozi Muadhamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na yanapaswa kuandaliwa kwa nguvu na fahari kubwa.

Aliongeza kuwa mashindano na maonesho ya kimataifa ya Qur’ani yanaonesha hadhi ya juu ya Qur’ani katika Jamhuri ya Kiislamu, na ni ishara wazi ya kipaumbele kinachotolewa kwa Qur’ani katika sera za kiutamaduni za taifa.

Maonesho ya Kimataifa ya Qur’ani ya Tehran huandaliwa kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu ya Iran.

Kwa vipengele mbalimbali kama vile vikao maalum, warsha za kielimu, mikusanyiko ya Qur’ani, na shughuli maalum kwa watoto na vijana, tukio hili la kimataifa linalenga kuendeleza dhana na shughuli za Qur’ani.

Maonesho haya pia ni jukwaa la kuonesha mafanikio ya hivi karibuni ya Qur’ani nchini Iran, pamoja na bidhaa mbalimbali zinazolenga kueneza na kuenzi Qur'ani Tukufu.

3495336

captcha