IQNA

Iran yalaani utekaji nyara uliofanyika Australia

14:16 - December 16, 2014
Habari ID: 2619145
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amelaani vikali utekaji nyara uliofanyika ndani ya mgahawa mmoja huko Sydney, nchini Australia.

Bi. Marziyeh Afkham amesema kuwa, Iran haikubaliki kutumiwa jina la dini tukufu ya Uislamu kwa lengo la kufanya mambo yaliyo dhidi ya ubinadamu na kusababisha hali ya hofu na wahka kwa jamii. Bi Afkham ameshangazwa na taarifa potofu na zisizo sahihi kuhusiana na mtekaji nyara huyo na kusema kwamba, mara kadhaa viongozi wa Iran waliwatahadharisha viongozi wa Australia kuhusiana matatizo ya kiakili aliyokuwa nayo mkimbizi huyo wa Kiirani aliyekuwa akiishi nchini Australia kwa karibu miaka ishirini.

Mtekaji nyara huyo aliyejulikana kwa jina la Man Haron Monis aliingia kwenye mgahawa wa Lindt Café mjini Sydney na kuwashikilia mateka watu kadhaa. Hata hivyo, jeshi la polisi lilifanikiwa kuwaokoa watu 17 waliokuwa wakishikiliwa mateka ndani ya mgahawa huo baada ya kutokea ufyatulianaji risasi uliopelekea watu watatu akiwemo mtekaji nyara kuuawa na wengine wanne kujeruhiwa.

Tony Abbott Waziri Mkuu wa Australia amesema kuwa, shambulio hilo la utekaji nyara limefanyika kwa malengo ya kisiasa. Duru mbalimbali zinasema kuwa, Haron Monis alikuwa mhalifu na mwenye historia ya kutenda jinai, zikiwemo za mauaji na ukatili wa kijinsia. Desemba Mosi mwaka huu Haron Monis aliituhumu Iran na nchi zinazounga mkono Rais Bashar Assad wa Syria kuwa ni magaidi.../mh

2618944

Kishikizo: haron monis Assad syria
captcha