Katika ujumbe kwa Rais Francois Hollande wa Ufaransa, Rais Rouhani amesema amesikitishwa na hujuma ya kikatili ya magaidi ambao wamewaua watu wasio na hatia mjini Paris. Rais Rouhani amesema, hakuna shaka ujumbe muhimu zaidi kwa dunia kufuatia hujuma hiyo ni kuimarika azma na irada ya mapambano ya pande zote katika kukabiliana na makundi ya kigaidi. Kwingineko msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sadeq Hussein Jabari Ansari amelaani vikali hujuma za kigaidi za Paris. Amesem magaidi hao watenda jinai hawafungamani hata kidogo na Uislamu wala dini nyingine yoyote ya mbinguni bali hata hawafuati misingi ya kimaadili na kibinadamu. Ameongeza kuwa hujuma hiyo ya kigaidi inatoa msukumo wa kuwepo irada imara ya kimataifa katika kukabiliana na kuangamiza ugaidi. Ansari amesema Iran imetangaza wazi sera zake za kupambana na ugaidi na misimamo mikali na kwamba itashirikiana na nchi zingine katika suala hilo.
Wakati huo huo Rais Hassan Rouhani wa Iran amevunja safari yake ya Ufaransa kufuatia hujuma ya kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Paris.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif leo Jumamosi akiwa katika uwanja wa ndege wa Mehrabad Tehran kabla ya kuelekea Vienna, Austria. Zarif ametangaza rasmi kuwa kufuatia hujuma ya kigaidi Paris, Rais Rouhani amefuta safari yake ya wiki hii Ulaya ambapo alitarajiwa kutembelea Italia na Ufaransa. Zarif ambaye pia amelaani hujuma hiyo ya ya kikatili Paris amesema Iran kama muathirika wa ugaidi daima iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuna haja ya kuwepo ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na ugaidi. Amesema dunia nzima inapaswa kuungana na watu wa Ufaransa na familia za waathirika wa hujuma hiyo ya kigaidi sambamba na kuchukua hatua za kuzuia kukaririwa tukio kama hilo siku za usoni. Zarif amekumbusha kuwa Rais wa Iran miaka miwili iliyopita katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alipendekeza kuundwa Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Misimamo mikali na Ugaidi kwa lengo la kukabiliana na ugaidi.