Nchini Iran, maadhimisho hayo ya kimaanawi yamefanyika kwa matembezi ya amani na marasimu katika misikiti na vituo mbalimbali vya kidini. Zaidi ya wafanyaziara milioni 2.5 wa Iran wameenda mjini Karbala Iraq kupitia vituo vitatu vya mpakani vya Mehran, Shalamcheh na Chazzabeh. Waziri wa Usafiri wa Iraq, Baqir al Zubeiri amesema kuwa, idadi ya wafanyaziara kutoka maeneo mbalimbali ya duniani waliowasili Karbala hadi hivi sasa imeshapindukia milioni 26. Habari zinasema kuwa, barabara ya Najaf kuelekea Karbala leo ilikuwa imefurika mamilioni ya wafanyaziara. Kwa mujibu wa shirika la habari la al-Sumaria la Iraq, jeshi la Iraq limefanikiwa kuangamiza magaidi 5 wa kujiripua kwa mabomu, waliokuwa na nia ya kuvuruga shughuli hiyo. Usalama umeimarishwa katika kila kona ya mji wa Karbala. Waandishi wa habari zaidi ya 600 kutoka vyombo vya habari zaidi ya 400 wanafuatilia tukio hilo la kimaanawi na kihistoria. Maadhimisho hayo kwa mara ya kwanza yalifanywa siku ya arubaini baada ya utawala wa Yazid kumuua shahidi Imam Hussein na wapenzi 72 wa watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume SAW katika jangwa la Karbala mwaka wa 61 Hijria. Tangu hapo kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS hufanyika kila mwaka.