IQNA

Mapingano yashadidi nchini Libya baina ya wanamgambo wa Haftar na jeshi la serikali

21:32 - April 14, 2020
Habari ID: 3472665
TEHRAN (IQNA)- Pamoja na kuwa janga la corona limeenea duniani kote na hivyo kupelekea kusitishwa mapigano katika maeneo mengi yamesitishwa lakini nchini Libya hali ni kinyume kwani tunashuhudia kushadidi vita.

Wanamgambo watiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar wameshadidisha hujuma ya maroketi dhidi ya mji mkuu Tripoli na wakati huo huo Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNU) siku ya Jumatatu ilitangaza kuwa imefanikiwa kudhibiti minane ya magharibi mwa Tripoli ambayo ilikuwa imetekwa na wanamgambo watiifu kwa Khalifa Haftar ambao wanajiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' (LNA).  Mohamed Qnounou msemaji wa  majeshi ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya alitoa taarifa na kusema miji iliyokombolewa ni pamoja Surman, Sabratha, Ajaylat , Al-Ajaylat, Regdaline, Al-Jmeil, Al Asa na Malit. Ameongeza kuwa: “Wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya wanawasaka wanamgambo wanaotoroka na wataendelea kusonga mbele kama sehemu ya Oparesheni ya Tufani.”

Miji hiyo iliyo kaskazini magharibi mwa Libya inahesabiwa kuwa ya kistratijia na serikali ya GNU kwa sababu kwa kuweza kuidhiiti, njia ya nchi kavu ya kuelekea katika mpaka wa nchi hiyo itaweza kufunguliwa tena.

Hali nchini Libya ni mbaya  na vita  vimeshadidi kwa kiasi kikubwa baina ya wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa na wanamgambo watiifu kwa Haftar.  Wanamgambo hao wa Haftar wanategemea uungaji mkono wa Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia na wanalenga maeneo mbali mbali ya Libya huku lengo lao kuu likiwa ni kuuteka mji mkuu Tripoli na kuchukua madaraka baada ya kuipindua serikali ya GNU.

Mashambulizi ya wanamgambo wa Haftar dhidi ya mji mkuu Tripoli yamepelekea wanajeshi wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya kuanza kutekeleza  ‘Oparesheni ya Tufani ya Amani’ dhidi ya wanamgambo hao. Lengo kuu la oparesheni hiyo ni kuchukua udhibiti wa maeneo yote ambayo yanakaliwa kwa mabavu na wanamgambo wa Haftar.

Vita vinazidi kupamba moto nchini Libya katika hali ambayo jamii ya kimataifa, hasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa wote wanaohusika na vita wavisitishe na badala yake wachukue hatua za kukabiliana na ugonjwa hatari wa corona.  Hadi sasa kumeshuhudiwa makumi ya kesi za maamubukizi ya corona nchini Libya na kutokana na vita wagonjwa hawajaweza kupata misaada na maisha yao yako hatarini.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

3471141

captcha