IQNA

Hali nchini Libya si shwari, jitihada za amani zaendelea

14:44 - June 07, 2020
Habari ID: 3472846
TEHRAN (IQNA) - Vita nchini Libya vimeshadidi na kushika kasi. Serikali ya Muafaka wa Kiataifa (GNU) yenye makao yake mjini Tripoli iko mbioni kukomboa maeneo yote ambayo yanakaliwa na wanamgambo wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar. Katika siku za hivi karibuni vikosi vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa vimepata mafanikio makubwa.

Siku chache zilizopita vikosi vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa nchini Libya vilifanikiwa kuudhibiti kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli na kufurusha mabaki ya wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftar. Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, Muhammad Qanunu amethibitisha kwamba, wapiganaji wa serikali wanaudhibiti kikamilifu mji wa Tripoli.  Aidha Qanunu amesema kuwa, jeshi la taifa sasa linadhibiti kikamilifu mji wa kistratijia wa Tarhuna ambao ulikuwa ngome kuu ya mwisho ya Khalifa Haftar huko magharibi mwa Libya. Amesema mji huo ulikombolewa kikamilifu mapema jana Ijumaa. Halikadhalika mji mwingine muhimu ambao umekombolewa ni ule wa Bani Walid ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Hatua ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa kuchukua udhibiti kamili wa mji mkuu Tripoli na maeneo ya karibu ni muendelezo wa kufeli mutawalia wanamgambo wa Haftar, mbabe wa kivita anayedhbiti maeneo ya mashariki mwa Libya.

Vita nchini Libya vimeshika kasi katika miezi ya hivi karibuni. Vikosi vya vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa  vinatekeelza oparesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la  Burkan Al-Ghadab au ‘Volkano ya Ghadhabu’ kwa lengo la kutoa pigo kwa wanamgambo wanaofungamana na Haftar wanaojiita ‘Jeshi la Kitaifa la Libya’. Oparesheni hiyo imepata mafanikio kwani maeneo mengi ambayo yalikuwa yametekwa na wanagamabo wa Haftar yamekombolewa. Kukombolewa maeneo ya kusini mwa Libya, Uwanja wa Ndege wa Tripoli na mji wote wa Tripoli ni mafanikio ambayo yameipa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa azma ya kuendelea kukomboa maeneo mengine yote yanayokaliwa na wanamgambo nchini humo.

Msemaji wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya, Muhammad Qanunu ametangaza kuwa: “Wanajeshi mashujaa wamepewa amri ya kuangamiza ngome zote za waasi  ambao hawapaswi kuhurumiwa hata kidogo. Libya itakuwa kaburi la wale wote  wanaoanzisha vita dhidi ya serikali. Wale wote wanaohatarisha usalama na uthabiti wa Libya na wanalenga kuiangusha serikali wantaangamizwa.

Ushindi wa vikosi vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya unajiri wakati ambao jitihada za kimataifa zingali zinaendelea kwa lengo la kuleta amani na kuanzisha tena mazungumzo baina ya pande hasimu nchini humo. Kuhusiana na hilo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa Libya, UNSMIL, imesema kumefikiwa mapatano baina ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa na wanamgambo wa Khalifa Haftar kuhusu kushiriki katika duru ya tatu ya mazungumzo ya Kamati ya Pamoja ya Kijeshi ya  “5+5” na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yatafanyika kwa lengo la kufikiwa mapatano ya usitishwaji vita.

Duru za kwanza na za pili za mazungumzo ya Kamati ya Pamoja ya Kijeshi ya  “5+5” zilifanyika mwezi Februari katika mji wa Geneva, Uswisi chini ya uwenyekiti wa Ghassan Salame, aliyekuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya kabla hajajiuzulu mwezi Machi. Mazungumzo hayo yaliwaleta pamoja wawakilishi watano wa ngazi za juu wa Serikali ya Muafaka wa Kiataifa Libya na wawakilishi watano wa  wanamgambo wa Haftar.  Hatahivyo hatua ya wapiganaji wa Haftar kukiuka mapatano na kuendelea mapigano ilipelekea mazungumzo yavunjike na vita nchini humo kushika kasi. Hatua ya Haftar kukiuka  Mapatano ya Skhairat na kuongezeka uingiliaji wa Misri, Imarati na Saudia, nchi ambazo zinamuunga mkono Haftar, kulipelekea hali ya Libya kuwa mbaya zaidi.

Hivi sasa mgogoro wa Libya umechukua muelekeo mpya. Kufichuliwa nyaraka za uingiliaji madola ya kigeni katika mgogoro wa Libya na pia kuingia pande mpya za kigeni katika uga wa kisiasa kumebadilisha kabisa mlingano katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Vita vya niaba nchini Libya vimeshika kasi na ingawa vikosi vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya vimepata ushindi mkubwa  na vinakaribia kupata ushindi wa mwisho na kuwadhoofisha kabisa wanamgambo na waasi, lakini hali ya kisiasa nchini Libya sambamba na kuwepo pande kadhaa za kitaifa na kimataifa ambazo zinataka kunyakua utajiri wa nchi hiyo ni kizingiti kikubwa katika kufikiwa utulivu na amani katika nchi hiyo. Kuhusiana na nukta hiyo, jamii ya kimataifa inaamini kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro wa Libya ni kupitia mazungumzo baina ya makundi yote nchini humo.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric anasema: “Ofisi ya Umoja wa Mataifa Libya, UNSMIL, ina matumaini kuwa pande zote  za kitaifa na kimataifa zitajibu takwa la wananchi wa Libya la kuhitimishwa mapigano na kuanza mazungumzo ya kamati ya kijeshi. Huu utakuwa mwanzo wa utulivu nchini Libya na hatua hii iandamane na mapatano ya kirafiki ya usitishwaji vita sambamba na kuandaliwa mazingira ya kufikiwa mapatano ya kudumu ya usitishwaji vita.

3471613

captcha