IQNA

Rais Raisi asema Iran inataka uhusiano mwema na nchi jirani

19:19 - September 01, 2021
Habari ID: 3474247
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia udharura wa kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na ushirikiano na mataifa jirani.

Rais Ibrahim Raisi amesema hayo leo katika kikao na baraza lake la mawaziri na kubainisha kwamba, kuongeza kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na ushirikiano wa Tehran na mataifa jirani ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya 13.

Sayyid Raisi ameongeza kuwa, udiplomasia amilifu kabisa wa serikali unapaswa kuelekezwa kwa mataifa jirani na Iran na kwamba, kuna haja ya kufanyika hima na juhudi zote kwa ajili ya kuongeza kiwango cha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi na majirani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matukio ya hivi karibuni nchini Afghanistan na kueleza kwamba, kile ambacho kimetokea kwa akali katika miongo miwili iliyopita katika nchi hiyo ni dhihirisho na ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu katika zama hizi.

Kadhalika Ibrahim Raisi amesema, tajiriba ya uwepo wa Marekani katika mataifa na maeneo tofauti ya dunia ni ushahidi wa wazi kwamba, uwepo huu hakuna wakati ambao ulileta amani bali kinyume chake kwani ulikuwa chimbuko la ukosefu  wa amani, usalama na utulivu katika maeneo hayo.

Kadhalika Rais mpya wa Iran amesema, kwa utendaji huu mbovu, Marekani badala itoe majibu mbele ya mahakama ya fikra za waliowengi ulimwenguni, sasa inatafuta visingizio na kuanzisha propaganda chafu dhidi ya mataifa mengine na kushupalia mambo hayo.

3994490

Kishikizo: iran Rais Raisi MAJIRANI
captcha