IQNA

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Rais wa Iran asema kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni kujitumbukiza shimoni

19:59 - October 01, 2023
Habari ID: 3477677
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, chaguo la kusalimu amri na kufanya mapatano kiudhalili halipo tena mezani na kwamba wale wanaoweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni kujitumbukiza kizazi.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo katika sherehe za ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, umoja uliopo leo hii baina ya Waislamu hauna maana ya kuunganisha madhehebu na kuishi katika eneo moja la kijiografia, bali ni umoja na mshikamano wa kulinda maslahi ya Umma wa Kiislamu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: "Adui hataki Umma wa Kiislamu uwe na umoja na mshikamano. Leo hii yeyote anayeelekea katika njia ya kuimarisha mshikamano na umoja huwa ametekeleza kivitendo mkakati wa dini tukukfu ya Kiislamu na iwapo atajaribu kuwafarakanisha Waislamu kwa kalamu na karatasi zake, huwa amejiingiza kwenye njia ya kufanikisha mkakati wa maadui."

Rais Raisi pia amesema, kuimarika harakati za ukombozi wa Quds tukufu na na ardhi zote za Palestina ni kielelezo cha wazi cha muqawama, mshikamano na kusimama imara umma wa Kiislamu na hiyo ndiyo njia bora zaidi hivi sasa ya kukabiliana na adui na tawala zinazofanya mapatano na adui huyo Mzayuni. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema, Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ni mkutano wa kupinga Uzayuni na utawala za kibeberu akabainisha kwamba, mkakati wa leo wa umoja na mshikamano katika safu za Waislamu unazidi kuufanya imara umma huo mbele ya adui na kwamba njia bora ya kushinda vita mseto vya adui ni umoja na mshikamano.

Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza kwa njia ya mtandaoni tarehe 28 mwezi ulioisha wa Septemba na utamalizika tarehe tatu mwezi huu wa Oktoba hapa jijini Tehran chini ya kaulimbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya Kufikia Matukufu Pamoja." Mkutano huo unafanyika kwa muundo wa ana kwa ana na kwa kupitia Intaneti.

4172310

Habari zinazohusiana
captcha