IQNA

Hujuma ya kigaidi

Ujumbe wa Rais wa Iran kufuatia hujuma ya kigaidi katika Haram ya Shah Cheragh

11:22 - August 14, 2023
Habari ID: 3477434
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Iran Ebrahim Raisi amewaagiza Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi na Gavana wa Mkoa wa Fars Mohammad Hadi Imaniyeh wawatambue haraka na kuwaadhibu wahusika wa shambulio la kigaidi katika Haram Takatifu ya Hadhrat Ahmad bin Musa (AS) maarufu kama Shah Cheragh mjini Shiraz kusini mwa Iran.

Katika mazungumzo tofauti ya simu, Raisi, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa (SNSC), amewataka maafisa hao wawili kutumia kikamilifu uwezo uliopo kwa ajili ya kuwahudumia waliojeruhiwa.

Raisi amesisitiza kuwa wale wote ambao kwa namna fulani wamehusika katika shambulio hilo la kigaidi lazima watambuliwe na kufikishwa mahakamani.

Ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia zilizofiwa na za waathiriwa.

Mtu mmoja aliuawa shahidi na wengine wanane kujeruhiwa jana jioni katika shambulio la kigaidi kwenye Haram Takatifu ya Shah Cheragh katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran.

Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti magaidi wawili walihusika katika ufyatuaji risasi siku ya Jumapili. Mmoja wa washambuliaji amekamatwa na mwingine anasemekana kuwa ametoroka. Watatu kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh lilidai kuhusika na hujuma hiyo mbaya.

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X ya mtandao wa kijamii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amelaani vikali shambulio hilo la kigaidi na kuonya kuhusu "mwisho wenye uchungu" kwa waliohusika na jinai hiyo.

Haram ya  Shah Cheragh huko Shiraz lilikuwa eneo la shambulio kama hilo la magaidi wenye silaha mwaka jana.

Mnamo Oktoba 26, 2022, gaidi mwenye silaha aliingia ndani ya eneo hilo la ibada, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama.

Gaidi huyo baadaye alifariki hospitalini kutokana na majeraha aliyopata.

Washukiwa kadhaa walikamatwa mara moja, na, wiki mbili baadaye, Wizara ya Usalama ilitangaza kukamatwa kwa magaidi 26 wakufurishaji waliohusika katika shambulio hilo.

4162313

Habari zinazohusiana
captcha