IQNA

Umoja wa Waislamu

Rais wa Iran: Umoja wa Waislamu ni kizuizi kwa madola ya kibeberu duniani

9:58 - September 01, 2023
Habari ID: 3477530
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ulimwengu wa Kiislamu ambao una umoja na mshikamano ndicho kizingiti kikubwa zaidi kwa ubeberu wa dunia.

Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran katika mkutano wake na wanazuoni wa Kisunni na kusisitiza kuwa, "Madola ya kibeberu yanautazama umma wa Kiislamu ulioungana kama kizingiti kikuu cha wao kufikia malengo yao katika enzi za baada ya Vita vya Pili ya Dunia."

Rais Raisi amebainisha kuwa, madola ya kiistikbari duniani yameweka vikwazo katika njia ya Waislamu kustawi, kwa kueneza propaganda kwa kutumia vyombo vya habari na kuunda makundi ya kigaidi na kitakfiri ili kusababisha umwagaji damu miongoni mwa Waislamu.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, maadui wanayavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kama kumtukana Mtume Muhammad (SAW) na kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ili kuchochea hisia za Waislamu duniani.

Kwengineko katika hotuba yake mbele ya wasomi wa Kiislamu wa madhehebu ya Sunni hapa mjini Tehran, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, wimbi la matukio yanayoshuhudiwa katika eneo linakwenda kwa maslahi ya kambi ya muqawama. "Hali ya sasa ya Palestina haiwezi kulinganishwa na kama ilivyokuwa huko nyuma," ameongeza Raisi.

Amebainisha kuwa, huko nyuma Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) iliwafanyia maamuzi Wapalestina, lakini hivi sasa maamuzi hayo yanachukuliwa na wanamuqawama wa Palestina.

Rais wa Iran ameongeza kuwa, nidhamu mpya ya dunia itaundwa kwa kusabaratika Marekani na madola ya kibeberu; na kwamba miungano kama ya BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai imesimama kidete dhidi ya mfumo wa ubeberu na sera zao za maamuzi ya upande mmoja.

 

4166176

Habari zinazohusiana
captcha