IQNA

Rais wa Iran afanya mazungumzo na viongozi wanaoshiriki kikao cha SCO nchini Tajikistan

22:53 - September 16, 2021
Habari ID: 3474303
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili katika mji mkuu wa Tajikistan, Dushanbe, ambako anashiriki mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) unaofanyika nchini humo leo na kesho.

Baada ya kuwasili Dushanbe, Rais Ebrahim Raisi amelakiwa na Waziri Mkuu wa Tajikistan, Kokhir Rasulzoda.

Hii ni safari ya kwanza ya Rais Sayyid Ebrahim Raisi nje ya nchi tangu alipochukua madaraka ya nchi baada ya kushinda uchaguzi wa Rais wa Juni mwaka huu. Rais Raisi ameelekea Tajikistan akiitikia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Emomali Rahmon na mbali na kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, vilevile anakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali wanaohudhuria mkutano huo. 

Habari zinasema Rais wa Jamhuri ya Kiislamu tayari amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan na Rais wa Uzbekistan, Shavkat Mirziyoyev.

Ajenda kuu ya mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu na viongozi hao imetajwa kuwa ni uhusiano wa pande mbili, uchumi, masuala ya kieneo na ushirikiano wa kimataifa.

Rais Ebrahim Raisi alitarajiwa pia kufanya mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake, Rais Emomali Rahmon.

Rais Ebrahim Raisi anafutana na ujumbe wa ngazi ya juu wa maafisa wa kisiasa na kiuchumi wa Iran katika safari hiyo huko Tajikistan.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai iliasisiwa mwaka 2001 kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na vitendo vya uchupaji mipaka na kuimarisha ushirikiana wa kiuchumi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni wanachama watazamaji katika jumuiya hiyo.

Stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya ushirikiano wa kieneo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya kisiasa na ushirikiano wa kiusalama, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni na kupanua ushirikiano wa muelekeo wa pande kadhaa kwa minajili ya kukabiliana na mtazamo wa upande mmoja wa ulimwengu wa Magharibi. 

3997938/

Kishikizo: iran ، rais raisi ، tajikistan ، SCO ، Pakistan
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha