IQNA

Diplomasia

Rais wa Iran kutembelea nchi tatu za Afrika kuimarisha uhusiano

17:40 - July 09, 2023
Habari ID: 3477261
TEHRAN (IQNA) Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi, anatazamiwa kuanza ziara rasmi ya kuzitembelea nchi tatu barani Afrika ili kuendeleza sera za Jamhuri ya Kiislamu za kuimarisha uhusiano na nchi marafiki.

Akiongoza ujumbe wa serikali ya Tehran, Raisi ataondoka Tehran kuelekea Kenya, Uganda na Zimbabwe siku ya Jumanne ijayo kwa mwaliko rasmi wa wenzake wa nchi hizo ili kujadili njia za kuboresha uhusiano wa kibiashara na kisiasa.

Katika ziara yake hiyo, Rais wa Iran atafanya mazungumzo na viongozi wenzake, kuhudhuria vikao vya wajumbe wa ngazi za juu, kushiriki katika mikutano na waandishi wa habari na kutia saini hati kadhaa za ushirikiano.

Vilevile atakutana na wafanyabiashara wa nchi hizo tatu pamoja na watendaji wa masuala ya uchumi na maafisa wa sekta mbalimbali ili kutumia fursa ya pamoja ya kiuchumi na kibiashara.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), hii itakuwa ziara ya kwanza ya Rais wa Iran barani Afrika baada ya miaka 11 ambayo inafanyika kwa kuzingatia sera ya mambo ya nje ya serikali ya sasa ya Tehran.

Safari ya Raisi inalenga kuimarisha uwepo wa Iran katika uchumi wa Afrika wenye thamani ya dola bilioni 600 kwa mujibu wa sera ya serikali ya sasa ya Tehran ya kuwepo ushirikiano wa pande nyingi za kiuchumi.

Chanzo: Press TV

Habari zinazohusiana
Kishikizo: Rais Raisi afrika iran
captcha