IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran itaunga mkono taifa madhulumu na la Waislamu Afghanistan

16:00 - August 28, 2021
Habari ID: 3474233
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaunga mkono taifa madhulumu la Waislamu la Afghanistan katika hali yoyote ile." Aidha ameongeza kuwa, uhusiano wa Iran na serikali zingine utategemea muamala wao na Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mkutano wake na Rais Ibrahim Raisi pamoja na baraza lake la mawaziri. Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa, nyuma ya pazia la udiplomasia wa Marekani pamoja na tabasamu  na matamshi ya kujiona mwenye haki ni mbwa mwitu wakali na wenye kuwinda," na kuongeza kuwa "Tab'an wakati mwingine pia hugeuka na kuwa mbweha mjanja na dhihirisho la hilo ni yale yanayojiri leo Afghanistan."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Afghanistan ni nchi ndugu ambayo ina  lugha, dini na utamaduni wa pamoja na Iran na huku akibainisha masikitiko yake makubwa kutokana na matatizo ya watu wa nchi hiyo ikiwemo hujuma ya hivi karibuni katika uwanja wa ndege wa Kabul amesema matatizo na masaibu hayo yamesababishwa na Marekani ambayo kwa miaka 20 imeikalia kwa mabavu nchi hiyo sambamba na kuwadhulumu watu wa nchi hiyo.

Ayatullah Khamenei amelihutubu baraza jipya la mawaziri Iran na kusisitiza ulazima wa kuwepo harakati maradufu katika sera za kigeni na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kuimarishwa muelekeo wa kidiplomasia katika sera za kigeni. Amesema kama ambavyo katika baadhi ya nchi rais ndiye ambaye hufuatilia udiplomasia wa kiuchumi, hapa nchini pia udiplomasia lazima uimarishwe.

Huku akisisitiza kuhusu udharura kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi 15 zinazopakana na Iran pamoja na nchi zingine za dunia, Kiongozi Muadhamu amesema: "Udiplomasia haupaswi kuathiri na kufungamanishwa na na kadhia ya nyuklia kwani maudhui ya nyuklia ni tafauti na ipanaswa kutatuliwa kwa njia ambayo inastahiki kwa nchi."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika kadhia ya nyuklia Wamarekani wamefikisha uhasama wao mbali sana na pamoja na kuwa waliondoka wazi wazi katika mapatano ya JCPOA mbele ya kila mtu lakini hivi sasa wanadai kuwa eti Iran ndiyo ambayo haijatekeleza majukumu yake katika JCPOA. Hii ni katika hali ambayo kwa muda mrefu baada ya Marekani kuondoka JCPOA Iran haikufanya chochote na baada ya hapo ilitangaza kusitisha tu baadhi ya ahadi zake na si zote katika mapatano hayo.

3993388

captcha