IQNA

Shakhsia Katika Qur’ani Tukufu /27

Firauni; mungu bandia aliyezama baharini

11:28 - January 15, 2023
Habari ID: 3476406
TEHRAN (IQNA) - Firauni lilikuwa jina la watawala wa Misri ya kale. Firauni aliyeishi wakati wa Nabii Musa (AS) alidai uungu. Alizama baharini lakini mwili wake umebaki kuwa fundisho kwa wanadamu.

Firauni alikuwa mtawala wa Misri yote na jemadari mkuu wa majeshi yake. Neno Firauni limetajwa katika Qur’ani Tukufu mara 74, na aya zote zinamtaja Firauni aliyeishi wakati wa Nabii Musa (AS).

Wanahistoria wengi wanaamini kwamba alikuwa Ramses II (1290-1224 KK) huku wengine wakisema ni Merenptah aliyetawala Misri kuanzia 1224 hadi 1214 KK).

Qur’ani Tukufu inamwelezea Firauni kama mtawala dhalimu aliyejiona  na kujigamba kuwa mungu wa Misri. Aliwaleta watu wa Bani Isra’il, walioishi Misri wakati wa utume wa Yusuf (AS), chini ya utawala wake. Kwa sababu wanajimu walikuwa wametabiri kwamba mvulana kutoka Bani Isra’il ataharibu ufalme wa Firauni, aliamuru kuuawa kwa watoto wote wa kiume wa Bani Isra’il. Hata hivyo, akihimizwa na mke wake Asiyah, Firauni alimchukua Musa kama mwanawe na akawa pamoja naye mpaka akawa kijana.

Firauni alikuwa hamwamini Mwenyezi Mungu. Angewafunga na kuwatesa wapinzani wake kwa njia mbalimbali.

Musa alipoteuliwa kuwa nabii, alipewa jukumu la kumwalika Firauni kwenye imani ya Mungu Mmoja yaani imani ya Tauhidi. Firauni alisikiliza yale aliyosema Musa na akaona miujiza yake pia lakini akaukataa wito wake na akamwita Musa kuwa ni mwongo na mchawi. Alimwomba Musa ashindane na wachawi wakuu wa Misri.

Wakati wa shindano hilo lililokuwa likifanyika siku ya mapumziko, wachawi hao waligundua kuwa alichokifanya Musa si uchawi. Lakini Firauni hakukubali, na akaamuru kuteswa kwa wachawi.

Musa na wafuasi wake walikimbia Misri usiku huku Firauni na watu wake wakiwafukuza. Walipofika baharini, Musa alinyoosha mkono wake na kunyoosha fimbo yake na Mungu akayagawanya maji, akawaruhusu wafuasi wake kupita kwa usalama. Lakini Firauni na watu wake walipofika na kuingia baharini, maji yakarejea na wakazama.

Qur’ani Tukufu inasema kwamba Firauni alikiri imani yake kwa Mwenyezi Mungu katika dakika ya mwisho kabla tu ya kuzama lakini haikukubaliwa. Qur’ani Tukufu pia inasema kwamba mwili wake uliokolewa ili uwe funzo kwa wengine: “Basi leo tutakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako ili uwe dalili kwa ajili ya wa nyuma yako. Na kwa kweli watu wengi wameghafilika na Aya zetu” (Surah Yunus, Aya ya 92)

captcha