IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /29

Talut; Mfalme wa Kwanza wa Bani Israil

18:38 - February 01, 2023
Habari ID: 3476501
TEHRAN (IQNA) – Bani Isra’il, ambao wakati wa utume wa Musa (AS) waliasi baadhi ya amri za Mwenyezi Mungu, waliendelea na uasi wao baada ya kifo cha Musa.

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa kumwacha mfalme mkandamizaji aliyeitwa Jalut awatawale. Lakini kwa uongozi wa Talut, walimaliza dhulma ya Jalut.

Talut alikuwa wa ukoo wa Benyamini, mwana wa Yaqub (AS). Talut aliishi karne tano baada ya Musa (AS). Aliishi na baba yake katika kijiji kilicho kando ya Mto Nile huko Misri. Inasemekana alikuwa mchungaji au mtengenezaji wa ngozi au muuza maji.

Baada ya kifo cha Musa (AS), Bani Isra’il waliendelea na uasi wao na wakafanya dhambi nyingi. Ili kuwaadhibu, Mwenyezi Mungu aliruhusu mfalme mkandamizaji atawale. Alikataa kufuata mafundisho ya Torati. Aliwalazimisha Bani Isra’il kutoka katika ardhi yao.

Baada ya miaka kadhaa, Mwenyezi Mungu alimteua Sham’un kama nabii na akamtuma kwa Bani Isra’il. Bani Isra’il walimwomba ateue kamanda wa kuwasaidia kupigana na Jalut.

Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, alimteua Talut kuwa kamanda. Hata hivyo, Bani Isra’il walipinga uteuzi huo kwa sababu mbili. Kwanza, kwa sababu wafalme na manabii wa Bani Isra’il daima walikuwa wa ukoo wa Lavi na Yuda, wana wa Yaqub, wakati Talut alikuwa wa uzao wa Benyamini. Na pili, walisema Talut hawezi kuwa kamanda mzuri kwa sababu hakuwa tajiri. Hii ilikuwa wakati Mwenyezi Mungu alikuwa amemchagua Jalut kama kamanda kutokana na elimu na uwezo wake.

Sham’un aliwaambia kwamba Talut alikuwa chaguo bora zaidi kwa sababu angeweza kurudisha “Sanduku la Agano”.

Hatimaye, walimkubali kama kamanda wao. Wakati Talut na jeshi la Bani Isra’il walipokwenda vitani, alipewa jukumu na Mungu kulijaribu jeshi hilo. Aliwaamuru wanajeshi kunywa maji kidogo tu ikiwa wana kiu kali wanapofika kwenye chanzo cha maji. Aliwaambia yeyote atakayekunywa zaidi ya hapo hataruhusiwa kuandamana na jeshi. Wengi wao waliasi na kushindwa kuandamana na Talut. Wafasiri wengine wamesema kwamba ni 500 tu waliobaki naye. Hata hivyo, kwa neema ya Mungu, jeshi hili dogo liliweza kupata ushindi katika vita.

Talut alikuwa ameahidi kwamba kama mtu yeyote anaweza kumuua Jalut, atamwoza binti yake na kumpa nusu ya mali yake.

Davoud (David) aliweza kuifanya. Kwa hiyo akapokea nusu ya mali ya Talut na akawa mkwe wake.

Imesemekana katika baadhi ya vyanzo kuwa kuelekea mwisho wa maisha yake, Talut alimwonea wivu Davoud na kuamua kumuua lakini akaachana na wazo hilo. Ili toba yake ikubalike, Talut alishiriki katika vita na aliuawa katika vita hivyo. Kulingana na vyanzo vingine, Talut alikufa kifo cha kawaida.

Jina la Talut na hadithi yake vimetajwa katika Surah Al-Baqarah ya Qur'ani Tukufu. Torati imemtaja Sauli. Wengine wamesema kwamba alikuwa mfalme wa kwanza wa Bani Isra’il na akawatawala kwa miaka 20 au 40.

captcha