Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na mamlaka za Bamako imeutaka Umoja wa Mataifa uviondoe vikosi vyake vya kulinda amani nchini Mali haraka iwezekanavyo 'bila kupoteza wakati.' Imesema sababu kuu ya kuwakataka askari hao waondoke ni 'mgogoro' wa ukosefu wa hali ya kuaminiana baina ya mamlaka za Mali na MINUSMA.
Watawala wa kijeshi nchini Mali wamekuwa wakivutana na Umoja wa Mataifa katika miezi ya hivi karibuni, hasa kuhusu kadhia ya askari hao wa kofia ya buluu wa UN.
Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Mali ilihoji usahihi na ukweli wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyodai kwamba kulikuwapo ongezeko kubwa la raia waliouliwa mwaka jana wa 2022, na kwamba jeshi la Mali lilihusika katika ukiukwaji huo wa haki za binadamu kwa zaidi ya theluthi moja.
Hata hivyo Bamako ilisema mwenendo wa ukusanyaji wa ripoti hiyo unaibua maswali mengi kuhusu uhalali na ukweli wa taarifa zote zilizokusanywa ndani ya ripoti hiyo.
Mwezi mwezi kabla, Bamako ilimfukuza Guillaume Ngefa-Atondoko Andali, Mkuu wa Idara ya Haki za Binadamu wa MINUSMA, kufuatia kile kilichotajwa na majenerali wa Mali kuwa utendaji usiofaa na wa upendeleo wa afisa huyo wa UN.
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali kinachojumuisha askari jeshi wa mataifa kadhaa (MINUSMA) kimekuwa kikidumisha usalama nchini humo tangu mwaka 2013.
Hata hivyo uwepo wa kikosi hicho umeshindwa kuzuia hujuma na mashambulizi ya makundi yenye silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la Daesh (ISIS) dhidi ya vijiji, miji, kambi za jeshi na vituo vya polisi nchini humo.