IQNA

Iran yaongeza maradufu idadi ya safari za ndege za Umrah

15:14 - September 26, 2025
Habari ID: 3481287
IQNA – Idadi ya safari za ndege zinazowasafirisha waumini wa ibada ya Umrah kutoka Iran kwenda Saudi Arabia imeongezeka tangu mwanzo wa wiki hii.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Hija na Umrah, safari nne za ndege za Umrah zinafanyika kila siku kutoka Iran kuelekea Ardhi ya Wahyi (Saudi Arabia).

Mwanzoni mwa msimu huu wa Umrah, ulioanza baada ya kumalizika kwa Hija, safari za ndege zilikuwa mbili kwa siku, na waumini walikuwa wakiondoka kupitia viwanja saba vya ndege.

Sasa idadi hiyo imeongezeka hadi safari nne kwa siku, na viwanja 10 vya ndege vimeongezwa katika mzunguko wa usafirishaji.

Kwa ongezeko hili la vituo na safari, takriban waumini 1,000 wa Kiirani wanasafiri kila siku kuelekea Saudi Arabia.

Sekta ya usafiri wa anga ina umuhimu mkubwa katika shughuli za Umrah, na inachangia karibu nusu ya gharama ya safari nzima.

Kwa sasa, safari zote za waumini wa Kiirani wanaotekeleza Umrah pekee zinaendeshwa na mashirika ya ndege ya ndani, na hadi sasa hakuna changamoto maalum zilizoripotiwa katika mzunguko wa usafirishaji wa mahujaji.

Katika tathmini ya mchakato wa Umrah wa mwaka uliopita, na kwa lengo la kuongeza kuridhika kwa wasafiri, msimu huu wa Umrah utahusisha kuwasafirisha waumini hadi viwanja vya ndege vya Jeddah na Madinah. Mwaka jana, mahujaji wote walitua katika uwanja wa ndege wa Jeddah pekee.

Kwa sasa, nusu ya waumini wanaelekea Madinah na baada ya kumaliza ibada yao, huondoka kupitia Jeddah. Nusu nyingine huanza safari yao kwa kutua Jeddah na kurejea kupitia Madinah.

Mpango wa Umrah wa mwaka huu unalenga kuhudumia waumini 200,000 kutoka Iran.

Umrah ambayo pia hujulikana kama Hija Ndogo ni ibada ya hiari (Mustahab) kuelekea Makkah, ambayo Muislamu anaweza kuitekeleza wakati wowote wa mwaka, tofauti na Hija ya faradhi ambayo ni wajibu kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha mara moja tu maishani, na hufanyika katika siku za mwanzo za mwezi wa Hijria wa Dhul-Hijjah.

3494752

Kishikizo: umrah saudi arabia iran
captcha