IQNA

Mwanaume akamatwa Singapore kwa kutuma kifurushi chenye nyama ya nguruwe kwenye Msikiti

17:55 - September 27, 2025
Habari ID: 3481293
IQNA - Polisi wa Singapore wamemkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 61 kwa tuhuma za kutuma kifurushi chenye nyama ya nguruwe kwa makusudi ya kuwadhalilisha Waislamu. Taarifa ya tukio hilo ilitolewa Septemba 24 baada ya kifurushi hicho kutumwa katika Msikiti wa Al-Istiqamah ulioko Serangoon North Avenue 2 saa 11:20 jioni.

Kifurushi hicho kilisababisha kuhamishwa kwa waumini waliokuwa msikitini kwa tahadhari. Mtu mmoja alikumbwa na hali ya kupumua kwa shida na alipelekwa katika Hospitali ya Sengkang, ambako baadaye aliruhusiwa. Hakuna kemikali hatari zilizogunduliwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mshukiwa alitambuliwa kupitia kamera za usalama na uchunguzi wa eneo la tukio, na alikamatwa siku iliyofuata. Ripoti ya Straits Times inaeleza kuwa huenda mwanaume huyo alihusika na matukio mengine ya aina hiyo katika misikiti mingine nchini Singapore.

Polisi wamethibitisha kuwa mshukiwa atafikishwa mahakamani Septemba 27 kwa kosa la kujeruhi hisia za kikabila kwa makusudi, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka mitatu, faini, au adhabu zote mbili.

Katika taarifa yao, polisi walisema: “Tunachukulia kwa uzito mkubwa vitendo vinavyotishia mshikamano wa kikabila na kidini nchini Singapore. Tabia kama hii haitavumiliwa na wahusika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.”

Waziri wa Mambo ya Ndani, K. Shanmugam, alieleza tukio hilo kuwa ni la kuchochea, bila kujali maudhui yake: “Haijalishi nia yake, hili ni kuchezea moto. Tutalishughulikia kwa uzito mkubwa.”

Tukio hilo limeibua kulaani kutoka kwa viongozi wa dini na makundi ya kijamii. Shirika la Ushirikiano wa Kidini (IRO) limesisitiza kuwa maeneo ya ibada lazima yawe “sehemu salama na za amani kwa wote.” Baraza la Kiislamu la Singapore (Muis) limewahimiza waumini kuwa watulivu wakati wa sala ya Ijumaa na kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa.

Wizara ya Utamaduni, Jamii na Vijana imepongeza uongozi wa msikiti kwa kuendelea na ibada licha ya tukio hilo, ikisema kuwa hatua hiyo inaonyesha mshikamano unaoelezea msimamo wa Singapore dhidi ya uchochezi wa aina hiyo.

Baraza la Ushauri la Wasikh pia limeeleza mshikamano wake na jamii ya Kiislamu, likilaani tukio hilo kwa kauli moja.

3494760

Kishikizo: singapore msikiti
captcha