IQNA

Mchochezi wa uchomaji wa nakala za Qur'ani Rasmus Paludan aepuka hukumu kamili nchini Sweden

20:51 - October 07, 2025
Habari ID: 3481338
IQNA – Mahakama ya rufaa nchini Sweden (Uswidi) imesitisha hukumu dhidi ya Rasmus Paludan, mwanasiasa wa mrengo wa kulia mwenye uraia wa Denmark na Sweden, ambaye amewahi kutukana na kuchoma nakala za Qur'an Tukufu mara kadhaa.

Mnamo Oktoba 6, Mahakama ya Rufaa ya Skåne na Blekinge ilimwondoa hatiani Paludan kwa sehemu, ikifuta moja kati ya mashtaka mawili aliyokuwa amehukumiwa mwaka 2022 kwa makosa ya chuki dhidi ya Waislamu kutokana na kauli alizotoa alipokuwa akichoma nakala za Qur'ani Tukufu. Mahakama hiyo ilisitisha kifungo chake cha miezi minne gerezani na kumtoza faini ya siku 50, kila siku ikiwa na thamani ya krona 50 (takriban KSh 1,000).

Wakati huo, Denmark na Sweden zilikuwa zikishuhudia maandamano ya hadhara ambapo wanaharakati wa kupinga Uislamu walikuwa wakichoma au kuharibu nakala za Qur'an, hali iliyozua ghadhabu katika ulimwengu wa Kiislamu na kuibua wito wa kuzuia vitendo hivyo.

Paludan, ambaye ni raia wa Denmark na Sweden, amewahi kuchoma Qur'an hadharani mara kadhaa, na wakati mwingine akiifunika kwa vipande vya nyama ya nguruwe. Ingawa kuchoma maandiko ya kidini kunaruhusiwa chini ya sheria za uhuru wa kujieleza nchini Sweden, uchochezi dhidi ya kundi la kikabila au kitaifa, kama vile kuwadhalilisha Waislamu, unaweza kuwa kosa la kisheria.

Kwa mujibu wa mahakama ya rufaa, kauli za Paludan za Aprili 2022 zinaweza kufasiriwa kama ukosoaji wa dini, jambo ambalo halihesabiwi kama uchochezi dhidi ya kundi la kikabila. “Kwa kuzingatia kuwa mwanasiasa huyo alikosoa Uislamu kama wazo katika sehemu nyingine za mkusanyiko huo, si dhahiri... kwamba kauli husika zinapaswa kufasiriwa kuwa zililenga kuwakosoa Waislamu kama kundi,” mahakama ilisema.

Tukio hili limeibua maswali makubwa kuhusu mipaka ya uhuru wa kujieleza na heshima kwa imani za kidini, hasa katika mazingira ya kisiasa na kijamii yanayozidi kuwa na migawanyiko. 

3494902

 

Habari zinazohusiana
captcha