IQNA

Hatua ya Mwisho ya Maonesho ya Kimataifa ya ‘Ulimwengu wa Qur’ani’ Yafikia Tamati Kazan

22:51 - October 08, 2025
Habari ID: 3481342
IQNA – Maonesho ya kimataifa ya Qur’ani yenye mwingiliano wa kisasa, yaliyopewa jina la “Ulimwengu wa Qur’ani”, yamehitimishwa rasmi mjini Kazan nchini Russia au Urusi mnamo Oktoba 6, baada ya kuyazunguka miji ya Moscow, Saratov, na Saransk.

Maonesho haya yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Uongozi wa Kiroho wa Waislamu wa Shirikisho la Russia na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar, yakifanyika katika Msikiti wa Marjani ulioko Kazan.

Kwa mujibu wa Realnoe Vremya, maonesho hayo yalijumuisha maonyesho ya kihistoria, filamu, shughuli za kielimu, na uzoefu wa hali halisi ya mtandaoni (virtual reality) uliolenga kuwakaribisha wageni wa kila asili na mazingira ya Qur’ani Tukufu.

Naibu Mwenyekiti wa Uongozi wa Kiroho wa Waislamu wa Urusi, Rushan Abbyasov, alisema mradi huo uliunganisha mbinu za ubunifu kutoka kwa washirika wote wawili, na kuzaa maonesho ya kipekee yenye sura nyingi. Baada ya mafanikio yake mjini Moscow, alieleza kuwa miji mingine ya Russia ilianza kuomba kuandaa maonesho hayo.

Ziara ya mwaka 2025 ilihusisha vituo katika Moscow, Saratov, na Saransk, na kuhitimishwa Kazan. Wakati wa ufunguzi, Mufti wa Tatarstan, Kamil Samigullin, aliwasilisha nakala ya Qur’ani iliyochapishwa na Khuzur Press, akipendekeza iongezwe kwenye mkusanyiko wa maonesho.

Sehemu muhimu ya maonesho hayo ilijikita katika historia ya uchapishaji wa Qur’ani mjini Kazan. Kazan Basmasy, iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1803, ilirudiwa kuchapishwa mara 165 kabla ya Mapinduzi ya Urusi. Nakala ya mwaka 1898 iliwekwa hadharani, na waandaaji wanapanga kuiongeza toleo la kisasa hivi karibuni.

Vitu vingine vya kipekee vilivyowekwa ni Qur’ani iliyochapishwa kwa maandiko ya Braille, nakala iliyosalimika wakati wa kuzingirwa kwa Leningrad, na mswada wa maandishi ya mkono kutoka mkoa wa Tambov. Maonesho pia yalieleza historia ya alama za kisarufi (diacritical marks) zilizotumika kuhakikisha usomaji sahihi wa Qur’ani kwa wasio wazungumzaji wa Kiarabu, hasa baada ya Uislamu kuenea nje ya ulimwengu wa Kiarabu.

Ghorofa ya pili ya maonesho ilihifadhi warsha za watoto na eneo la hali halisi ya mtandaoni lililotengenezwa na wataalamu wa Qatar. Uzoefu wa VR uliwawezesha washiriki kutembelea Makkah, Madinah, na hata ndani ya Kaaba, kwa kuzingatia kanuni za sanaa ya Kiislamu zinazokwepa kuchora watu au wanyama.

Katika kipindi chote cha maonesho, wageni walipata vyeti kwa kukamilisha shughuli za kielimu kama vile kufuatilia maandishi ya Kiarabu ya kisanaa (calligraphy) au kusoma Surat al-Fatiha, sura ya kwanza ya Qur’ani. Kila siku kulikuwa na maonyesho ya filamu fupi na za maandishi, ikiwemo “Historia ya Qur’ani: Kutoka Ufunuo hadi Maandishi” na “Al-Khwarizmi maaruru kama Baba wa Hisabati.”

 Waandaaji tayari wamepokea mialiko ya kupeleka maonesho hayo katika maeneo ya Caucasus, Siberia, na Mashariki ya Mbali mwaka 2026.

Maonesho hayo yalichukua ghorofa mbili za upande wa kulia wa msikiti. Mabango makubwa ya ghorofa ya kwanza yalieleza jinsi Qur’ani ilivyoteremshwa, kukusanywa, na kuhifadhiwa.

 

3494922

Habari zinazohusiana
captcha