Kwa mujibu wa agizo lililotolewa, Sheikh Ikrima Sabri, ambaye ni miongoni mwa wahubiri mashuhuri wa Msikiti wa Al-Aqsa, amepigwa marufuku kuingia katika eneo la msikiti au kuongoza swala kwa kipindi cha miezi sita. Mashirika ya haki za binadamu yameeleza kuwa agizo hili ni mwendelezo wa kampeni ya kimfumo ya utawala wa Kizayuni ya kuwadhibiti na kuwanyamazisha viongozi wa Kiislamu wenye ushawishi katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Katika taarifa rasmi, Baraza Kuu la Kiislamu limesema: “Utawala wa Kizayuni umetangaza marufuku dhidi ya Sheikh Ikrima Sabri kuingia Msikiti wa Al-Aqsa na kuswali humo kwa muda wa miezi sita; hatua hii ni sehemu ya mfululizo wa maamuzi na ukiukaji dhidi ya Sheikh Sabri.”
Baraza hilo limeeleza kuwa hatua hiyo ni “uvunjaji mkubwa na usiovumilika wa haki za kidini,” likisisitiza kuwa Sheikh Sabri ni “mamlaka muhimu ya Kiislamu katika ardhi ya Palestina.” Kwa mujibu wa Jordan News, baraza hilo limeonya kuwa marufuku hiyo ina athari nzito za kidini na kisiasa, na likatoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kuchukua msimamo madhubuti dhidi ya ukiukaji unaoendelea wa uhuru wa kuabudu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa utawala wa Kizayuni “unachochea vita vya kidini” kupitia vitendo vyake katika maeneo matakatifu, na kwamba mashinikizo dhidi ya maimamu na waumini wa Al-Aqsa yameongezeka chini ya serikali ya mrengo wa kulia.
Kamati ya utetezi ya Sheikh Sabri imesema kuwa vitisho na usumbufu dhidi yake vimekuwa vikifanyika kwa miaka mingi licha ya hadhi yake ya juu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kamati hiyo imeeleza kuwa Israel “inaendelea kumlenga Sheikh Sabri bila kuwajibika kimataifa,” na kuchochea chuki kupitia vyombo vya habari vya Kizayuni. “Baadhi ya wachambuzi wa mrengo mkali wamefikia hatua ya kuhimiza vyombo vya usalama kumuangamiza badala ya kumhoji,” kamati hiyo imeonya, ikieleza kuwa kauli hizo ni “njama ya polisi, uvunjaji wa sheria, na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.”
Sheikh Sabri, ambaye amehudumu kama kiongozi wa juu wa Kiislamu kwa zaidi ya miaka hamsini, amekuwa akitiwa nguvuni na kupigwa marufuku mara kwa mara kuingia Al-Aqsa katika miaka ya hivi karibuni. Amekuwa mkosoaji wa wazi wa uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina na ameonyesha uungaji mkono thabiti kwa watu wa Gaza wanaokabiliwa na mashambulizi yasiyokoma.
Kamati ya utetezi imesisitiza kuwa Sheikh Sabri “hapaswi kuadhibiwa kwa kutekeleza majukumu yake ya kidini,” ikieleza kuwa sauti yake ni ya heshima na inawakilisha urithi wa Kiislamu wa al-Quds.
3494906