IQNA

Al-Azhar ya Misri yazindua Apu ya kufundisha Qur’ani Tukufu

17:08 - October 02, 2025
Habari ID: 3481318
QNA – Kwa jitihada za vituo vinavyohusiana na Al-Azhar nchini Misri, programu maalumu ya kufundisha Qur’ani Tukufu imezinduliwa kwa lengo la kuhudumia Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu.

Aplikesheni au Apu hii inayojulikana kwa jina la “Msomaji wa Qur’ani wa Kielektroniki” imetengenezwa kwa msaada wa Sheikh Mkuu wa Al-Azhar, Ahmad Al-Tayyib, na chini ya usimamizi wa Naibu wake, Muhammad Abdul Rahman Al-Duwaini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kituo hicho cha Kiislamu kunufaika na teknolojia za kisasa kwa ajili ya kuhifadhi na kufundisha Qur’ani Tukufu.

Kikundi cha wataalamu wa programu kutoka taasisi zilizo chini ya Al-Azhar kimehusika katika kutengeneza programu hii, ambayo imelenga kusaidia wanafunzi na walimu kusoma Qur’ani kwa usahihi na kwa tajwidi sahihi.

Idara Kuu ya Masuala ya Qur’ani ya Al-Azhar imefanya tathmini ya kiufundi ya programu hiyo ili kuhakikisha usahihi wa usomaji, uhalali wa maudhui, na ufuatiliaji wa kanuni za tajwidi.

Apu hii ni chombo chenye nguvu cha kielimu kinachosaidia mchakato wa kufundisha Qur’ani ndani na nje ya taasisi za Al-Azhar, kwa kuweka mazingira bora ya usomaji sahihi na wazi wa Qur’ani Tukufu.

Mradi huu umetekelezwa kwa mujibu wa dhamira ya Al-Azhar ya kuimarisha matumizi ya zana za kisasa za kiteknolojia katika elimu ya dini, jambo ambalo litasaidia kuimarisha maadili ya Kiislamu na kurahisisha kuhifadhi na kusoma Qur’ani Tukufu, kwa mujibu wa maelezo ya kituo hicho cha Kiislamu.

3494828

captcha