IQNA – Uchunguzi wa uhalifu wa chuki unaendelea baada ya chupa ya pombe kurushwa kupitia dirisha la mlango wa msikiti mmoja mjini Montreal, Canada. Polisi wa jiji wamekabidhi kesi hiyo kwa kitengo chao cha uhalifu wa chuki na kuomba umma kutoa taarifa.
Konstebo Jean-Pierre Brabant alithibitisha kuwa tukio hilo lilitokea wakati fulani kati ya saa 3 usiku Jumamosi na saa 11:30 alfajiri Jumapili katika Msikiti wa Al Qods, kwenye Mtaa wa Bélanger, karibu na Barabara ya Louis-Hébert, katika kata ya Villeray–St-Michel–Parc-Extension.
“Hakuna aliyekamatwa kufikia sasa,” alisema alasiri ya Jumatatu.
Kwa mujibu wa Brabant, mtu mmoja aliripoti tukio hilo karibu saa 6:40 mchana Jumapili.
Alieleza kuwa bado haijabainika kama msikiti huo ulilengwa kwa uhalifu wa chuki.
“Tutalichunguza ili kuona kama kuna taarifa yoyote inayoweza kutuonyesha au kutuelekeza kwenye uhalifu wa chuki,” alisema Brabant, akiongeza kuwa polisi “hawachukui hatari yoyote.”
“Tutachunguza taarifa zote tulizonazo. Tutakutana na mmiliki ili kuona kama kulikuwa na ... vitisho vya awali au jumbe zilizotangulia,” aliongeza, akisema kuwa msikiti huo umewahi kulengwa huko nyuma na matukio hayo nayo yalichunguzwa na kitengo cha uhalifu wa chuki.
Ndani ya msikiti, swala za kila siku zilikuwa zikiendelea Jumatatu.
Muumini mmoja aliiambia The Gazette kuwa ilikuwa chupa ya pombe iliyorushwa kupitia dirisha la mlango. Kufikia alasiri ya Jumatatu, dirisha lililovunjika lilikuwa limefunikwa, na vipande vya kioo vya kile kilichoonekana kuwa chupa ya vermouth vilikuwa vimeng’oliwa na kuwekwa kwenye sanduku la kadibodi.
Polisi watatafuta picha za kamera za uchunguzi za tukio hilo, na doria zitaongezwa katika eneo hilo, kwa mujibu wa Brabant.
/3499734