IQNA

Kanisa labadilishwa na kuwa msikiti nchini Canada

20:44 - February 22, 2021
Habari ID: 3473674
TEHRAN (IQNA)-Jengo la Kanisa la St. James Presbyterian mjini Ontario nchini Canada limebadilishwa na kuwa msikiti baada ya kununuliwa na Waislamu.

Kwa mujibu wa taarifa, Waislamu wa mtaa wa Chatham mjini Ontario wamekuwa wakitaka eneo lao la kuswali kwa muda mrefu na  sasa kwa msaada wa Kituo cha Kiislamu cha Chatham wameweza kununua kanisa ambalo halikuwa na watumizi na wamligeuza kuwa msikiti.

Amir Naveed, Rais wa Kituo cha Kiislamu cha Chatham amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikodisha maeneo ya kuswali na walikumbwa na matatizo mengi kwa sababu ya ukosefu wa nafasi ya kutosha katika maeneo yaliyokodiwa.

Ameongeza kuwa mwaka 2019 walianza kutafuta jengo la kudumu  na hatimaye waliweza kupata jengo hilo la kanisa ambalo wamiliki wake walikuwa tayari kuliuza. Naveed anasema jengo hilo la kanisa halikufanyiwa mabadiliko mengi kabla ya kuanza kutumika kama msikiti.

Kwa ujumla Canada ni nchi ambayo huwakaribisha wahamiaji na wafuasi wa dini zote lakini katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Pamoja na hayo Waziri Mkuu Justin Trudeau amesema Waislamu nchini Canada wamekuwa na mchango mkubwa  nchini humo na hivyo hatua zitachukuliwa kwa wale wanaoeneza chuki dhidi ya Uislamu.

/3474054

Kishikizo: canada ، msikiti ، kanisa ، ontario
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha