IQNA

Maombolezo baada ya Waislamu wanne kuuawa Canada kwa kukanyagwa na gari kwa makusudi

20:42 - June 08, 2021
Habari ID: 3473988
TEHRAN (IQNA)- Maombolezo yanafanyika baada ya dereva mmoja mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Canada kuua watu wanne wa familia moja na kujeruhi mwingine vibaya, baada ya kuwagonga kwa makusudi na lori lake katika mkoa wa Ontario.

Polisi katika mkoa huo jana Jumatatu ilithibitisha kuwa watu hao waliuawa kutokana na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ya dereva aliyetekeleza unyama huo katika mji wa London, kusini magharibi mwa mkoa wa Ontario.

Kadhalika meya wa mji wa London katika mkoa huo wa Ontario kulikotokea shambulizi hilo la chuki dhidi ya Uislamu, Ed Holder ameutaja ukatili huo kama mauaji ya umati dhidi ya Waislamu.  Amesema, "mzizi wa mauaji hayo ni chuki za dhati zisizo na kifani. Ukubwa wa chuki hiyo unafanya mtu ajiulize, sisi ni nani (watu wa aina gani) kama jiji." 

Msikiti wa The London Muslim Mosque umeandaa khitma kwa ajili ya kuomboleza mauaji ya kikatili ya Waislamu hao.

Polisi wamesema waliopoteza maisha katika hujuma hiyo ya kigaidi ni pamoja na  Salman Afzaal, 46, na mke wake aliyekuwa na umri wa miaka  44 Madiha Salman, binti yao Yumna Salman aliyekuwa na umri wa miaka 15 na  mama yake Afzaal aliyekuwa na umri wa miaka 74.

Mtoto wao mvulana, Fayeza mwenye umri wa miaka 9 amejeruhiwa vibaya na sasa amelazwa hospitalini.

Wakati huohuo, Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada kupitia ujumbe wa Twitter amelaani vikali mauaji hayo aliyoyataja kuwa yamechochewa na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).

Kijana wa miaka 20, Nathaniel Veltman, aliyetekeleza unyama huo ametiwa mbaroni, na kufunguliwa mashitaka manne ya kuua kwa kukusudia, na shitaka moja la jaribio la kuua.

Vitendo vya ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu nchini Canada vimeshtadi katika miezi ya hivi karibuni. Septemba mwaka jana, Baraza la Kitaifa la Waislamu nchini Canada lilitoa mwito wa kuchunguzwa mauaji ya Muislamu nje ya msikiti mmoja mjini Toronto, na kusisitiza kuwa mauaji hayo yalichochewa na chuki za kidini.

Waislamu nchini humo wamewahi kumuandikia barua Waziri Mkuu Justin Trudeau wakimtaka aitangaze Januari 29 kuwa 'Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Chuki na Kutovumiliana' baada ya kushtadi vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

3474921

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha