Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, magaidi waliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa katika msikiti wa Kituo cha Kiutamaduni cha Quebec, wakati wa Sala ya Ishaa saa mbili usiku kwa wakati wa Quebec ( 0100 GMT Jumatatu).
Polisi katika eneo la Quebec wanasemea watu wengine 8 walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi ambapo gaidi moja tayari ameshakamatwa kufuatia tukio hilo.
Kulikuwa na watu 50 ndani ya kituo hicho cha Kiislamu wakati wa hujuma hiyo huku ripoti zikisema watu tano yati ya waliojeruhiwa wako katika hali mahututi wakiwa wamelezwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Quebec.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amelaani hujuma dhidi ya msikiti huo na kuitaja kuwa ya kigaidi. "Tuko pamoja nanyi” Trudeau amewaambia Waislamu zaidi ya milioni moja wa Canada alipohutubu bungeni Jumatatu. Aliongeza kuwa waliopoteza maisha na kujeruhiwa wamelengwa kwa ajili ya dini yao. Amewahakikishia Waislamu kuwa Wacanada wote milioni 36 wako nao na wanawathamini.
Kituo cha Kiutamaduni cha Kiislamu mjini Quebec kimekuwa kikilengwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) mara kwa mara. Mwezi Juni mwaka jana wakati wa Ramadhani, watu wenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu waliacha kichwa cha nguruwe katika mlango wa msikiti huo.
Aidha mwaka 2015, msikiti mmoja katika jimbo la Ontario nchini Canada uliteketezwa moto na watu wenye misimamo ya kurufutu ada wanaouchukia Uislamu.
Kwa ujumla Canada ni nchi ambayo huwakaribisha wahamiaji na wafuasi wa dini zote lakini eneo linalozungumza kifaransa la Quebec limekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu kuwakubali watu wa rangi na dini mbali mbali. Serikali iliyopita ya Quebec ,ambayo ilikuwa ikipigania kujetenga eneo hilo na Canada, ilikuwa imetaka vazi la wanawake Waislamu la Hijabu lipigwe marufuku katika taasisi za umma.