Jeshi la Polisi la Peel limesema lilipokea taarifa za uharibifu uliofanywa katika Kituo cha Kiislamu kilichopo eneo la Montevideo Road mnamo saa 7 usiku, Agosti 15. Afisa wa habari wa polisi, Konstebo Tyler Bell-Morena, amesema tukio hilo linachunguzwa na kitengo cha makosa ya chuki, lakini bado ni mapema kusema kama lilichochewa na chuki dhidi ya Uislamu.
“Kwa sababu ni kituo cha Kiislamu, na kwa kuzingatia unyeti wa eneo hilo, ni mahali pa ibada, mahali ambapo Waislamu hukusanyika , bila shaka tunazingatia uwezekano wa chuki,” alisema Bell-Morena alipokuwa akizungumza na CBC Toronto.
Taarifa za kamera za usalama zilizoonekana na CBC zinaonyesha mtu mmoja akivunja milango ya kioo ya mbele ya Kituo cha Kiislamu cha Ar-Rehman kwa kutumia kifaa kinachofanana na skateboard au longboard. Mshukiwa huyo alifanya vivyo hivyo kwa kituo cha misaada cha Kiislamu kilicho jirani, ICNA Relief Canada, kisha akaondoka kwa miguu.
Kwa bahati nzuri, mtu huyo hakufanikiwa kuingia ndani ya majengo hayo na hakuna majeruhi walioripotiwa, kwa mujibu wa Bell-Morena. Polisi bado hawajamtambua mshukiwa kwa jina, lakini wanashirikiana na wanajamii waliodai kumwona mtu huyo hapo awali.
Ingawa kitengo cha makosa ya chuki kinachunguza tukio hilo, polisi wanasema mshukiwa anatafutwa kwa kosa la uharibifu wa mali. Bell-Morena alisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa kina: “Si kila tukio linalotokea katika taasisi za kidini linachochewa na chuki, ingawa mengine huwa hivyo. Kila tukio la chuki ni kosa la jinai, lakini si kila kosa la jinai linachochewa na chuki.”
Jamii Yatishwa
Baadhi ya wanajamii wameingiwa na hofu, amesema Minhaj Qureshi, Mwenyekiti wa ICNA Canada Mississauga. “Kuna hofu miongoni mwao. Wanauliza kama tuko salama hapa au la,” alisema Qureshi.
Qureshi anaamini tukio hilo lilichochewa na chuki na amekosoa polisi kwa kutotoa taarifa zaidi kuhusu uchunguzi huo. “Anauliza: Polisi wanafanya nini? Hadi sasa hatujapata taarifa yoyote kuhusu iwapo mtu huyo amekamatwa au la. Tunataka haki. Tunataka usawa. Hilo ndilo tuntalodai, hatudai kingine.”
Aidha, Qureshi anashangaa kwa nini polisi hawajatoa picha au video ya mshukiwa hadi sasa. “Ni siku kumi na mbili zimepita, lakini bado hawajatoa picha hiyo,” alisema.
Bell-Morena alijibu kuwa sababu ya kutotoa taarifa ni kwa kuwa wachunguzi wanaamini hakuna tishio kwa umma kwa sasa. “Iwapo ingekuwa shambulio la moja kwa moja dhidi ya mtu binafsi, tungechukua hatua za haraka zaidi kwa kuhusisha umma,” alisema.
“Wachunguzi wanataka kumpata mtu huyu na kwa sasa wanafuatilia nyendo fulani za uchunguzi. Wakati mwingine wanapaswa kupima kati ya kushikilia taarifa na kuitoa hadharani, kwa sababu kutoa mapema kunaweza kuathiri mikakati yao.”
3494422