IQNA

Mamia ya watu Canada washiriki katika maombolezo ya Waislamu waliouawa

15:05 - June 10, 2021
Habari ID: 3473995
TEHRAN (IQNA)- Mamia ya waombolezaji walikusanyika Jumanne usiku katika mtaa wa London, mjini Ontario Canada kuwaomboleza Waislamu wanne waliuawa katika tukio la chuki dhidi ya Uislamu.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amejiunga katika maombolezaji ya Waislamu hao na kusema yuko pamoja  na kila aliyeumizwa na mauaji hayo.

Vyombo vya habari vya Canada Jumatatu ya juzi viliripoti kuwa, dereva mmoja mwenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo ameua watu wanne wa familia moja na kujeruhi vibaya mwingine, baada ya kuwagonga kwa makusudi na lori lake katika mkoa wa Ontario. Polisi katika mkoa huo wamethibitisha kuwa, watu hao waliuawa kutokana na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ya dereva aliyetekeleza unyama huo katika mji wa London, Kusini Magharibi mwa jimbo la Ontario.

Kijana mwenye umri wa miaka 20, Nathaniel Veltman, aliyetekeleza unyama huo amefunguliwa mashitaka manne ya kuua kwa makusudi, na shitaka moja la jaribio la kuua. Polisi ya Canada inasema chuki za kidini ndiyo sababu ya hujuma hiyo.

Waliouawa katika shambulizi hilo wametajwa kuwa ni baba wa familia, Salman Afzal, 46; mke wake Madiha, 44; binti yao Yumna, 15; na bibi aliyekuwa na umri wa miaka 74 ambaye jina lake limehifadhiwa. Mtoto mdogo wa kiume wa familia hiyo, Fayez, 9, amejeruhiwa vibaya na amelazwa hospitalini.

Ushahidi unaonesha kuwa hatua hiyo ya kigaidi ilipangwa tangu hapo awali na si tukio la sadfa. Takwimu zilizotolewa na Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 kumefanyika hujuma na mashambulizi 300 dhidi ya Waislamu nchini humo na kwamba, zaidi ya mashambulizi 30 yaliambatana na ukatili mkubwa. Miongoni mwa mashambulizi hayo ni lile lililolenga msikiti katika mkoa wa Quebec mwaka 2017 na kuua Waislamu 6 waliokuwa wakitekeleza ibada.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ya kupambana na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kilia ni maneno matupu yaliyotolewa kwa ajili ya kutuliza hasira za Waislamu ambao wanaendelea kusumbuliwa na manyanyaso na ubaguzi wa kimfumo katika nchi za Magharibi. 

3976392

 

Kishikizo: canada ، waislamu
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* :