IQNA

Madola ya 5+1 yafidie makosa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

10:33 - November 16, 2013
Habari ID: 1317806
Khatibu wa sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran amesema kuwa, kundi la 5+1 linapasa kutumia vyema fursa iliyopo ya mazungumzo ya nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili kufidia makosa liliyoyafanya huko nyuma dhidi ya taifa la Iran.

Hujjatul - Islam Kadhim Siddiqi amesisitiza kuwa, iwapo kundi la 5+1 litaingia kwenye mazungumzo hayo kwa kutumia njia za mantiki, hekima na ukweli kama ilivyo kwa Iran, bila shaka kadhia hiyo itamalizika kwa maslahi ya pande mbili za mazungumzo hayo. Hujjatul Islam Siddiqi amesema kuwa, maamuzi yoyote yatakayochukuliwa kwenye mazungumzo ya nyuklia yanapasa kuhifadhi maslahi ya taifa na moyo wa hamasa wa wananchi wa Iran. Aidha amewataka vijana wa Kiirani kupiga hatua zaidi katika kujipatia maendeleo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo teknolojia ya nyuklia. Huku akizitahadharisha baadhi ya nchi zinazofanya njama za kutaka kukwamisha mazungumzo hayo, Sheikh Siddiqi ameongeza kuwa nchi hizo zinapasa kuelewa kwamba kuvunjika mazungumzo hayo hakutauathiri hata chembe moyo wa kujitawala wa wananchi wa Iran. Khatibu wa sala ya Ijumaa ya Tehran amekumbushia tukio chungu la kihistoria la  kuuawa shahidi Imam Hussein AS na wafuasi wake katika ardhi ya Karbala,  pamoja na siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam  Ali bin Hussein Zainul Abidin AS na kusema kuwa, Imam Zainul Abidiin AS aliweza kutekeleza majukumu yake vilivyo ya kuuongoza umma wa Kiislamu, baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Hussein AS.

1317618
captcha