Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, mashindano hayo yamewaleta pamoja washiriki kutoka maeneo ya Kibra na Kawangware na imearifiwa kuwa washiriki 20 wameshiriki katika awamu hii ya mashindano ya Qur’ani yanayofanyika kwa himaya ya Idara ya Utamaduni ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi.
Mashindano hayo yalianza kwa hotuba ya Imamu wa Masjid Kambi, Sheikh Yusuf Nasoor ambaye alisema lengo kuu la mashindano ya Qur’ani si kupata mshindi au mshindwa bali ni kustawisha utamaduni wa usomaji, ufahamu na kuhifadhi Qur’ani Tukufu.
Aliongeza kuwa Allah SWT amesema, ‘mbora miongoni mwenu ni yule ambaye anajifunza na kuifunza Qur’ani’ na hivyo aliwatakia wote mafanikio katika mashindano hayo.
Hotuba ya pili ilitolewa na Bw. Mwinyi Ramadhani, afisa mwandamizi katika Idara ya Utamaduni ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi ambaye pia alisistiza kuwa lengo la mashindano ni kusimarisha utamaduni wa usomaji wa Qur’ani Tukufu.
Aidha aliongeza kuwa mashindano hayo ya mchujo yanafanyika pia kwa minajili ya kumtafuta hafidh na qarii ambaye ataiwakilisha Kenya katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani yatakayofanyika Iran mwezi Mei mwaka huu wa 2014.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Sheikh Omar Mwamtunza ambaye aliwataka washiriki kuzingatia kanuni na ahkam za usomaji Qur’ani kama vile sauti, lahni na makharij.
Hadhrina pia walihutubiwa na Mkurugenzi wa Madrassatul Ulumul Islamiya Kibra ambayo ni kitengo cha Masjid Kambi Sheikh Juma Khamis. Katika hotuba yake Sheikh Khamis aliishukuru kwa dhati Idara ya Utamaduni ya Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ameyataja kuwa muhimu kwa Ummah wa Kiislamu. Aliwahimiza Waislamu kuisoma Qur’ani na kuongeza kuwa ‘iwapo utakuwa rafiki wa Qur’ani, Qur’ani itakuwa rafiki yako na kuwa shahidi wako katika Siku ya Qiyama.’
1389803