Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kwamba, adui anachochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq na kuwapiganisha Shia na Suni ili kukabiliana na wimbi la mwamko wa Kiislamu. Akizungumza Jumamosi hii, Ayatullah Khamenei aliashiria mgogoro unaoendelea nchini Iraq na kusema kuwa, mabaki ya utawala uliopinduliwa wa dikteta saddam Hussein na kundi la watu wajinga na majahili wanatekeleza jinai katika nchi hiyo. Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba, kinachojiri nchini Iraq si vita kati ya Shia na Suni bali ni vita vya ugaidi na wanaounga mkono nchi za Magharibi dhidi ya wapinzani wa ugaidi na watetezi wa uhuru wa mataifa mbalimbali. Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo akihutubia familia za mashahidi waliopoteza maisha kwenye shambulio la bomu la kigaidi ulililotokea tarehe 7 Tir mwaka 1360 wa Kiirani sawa na Juni 1981. Watu 72 wakiwemo mawaziri na wabunge 72 wa Iran walipoteza maisha katika mlipuko huo akiwemo Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliyekuwa Mkuu wa Mahakama za Iran.