IQNA

Mfungwa wa Kipalestina aliyeachiliwa azungumzia udhalilishaji wa Qur'an katika Magereza ya Israel

21:11 - October 26, 2025
Habari ID: 3481418
IQNA – Mfungwa wa Kipalestina aliyeachiliwa kutoka gereza la utawala wa Kizayuni ameeleza mateso makali na hali isiyo ya kibinadamu inayowakumba wafungwa wa Kiislamu, ikiwemo udhalilishaji wa Qur'an Tukufu na kuzuia adhana na sala za jamaa.

Anas Allan, mzaliwa wa Qalqilya katika Ukingo wa Magharibi, alifichua mateso ya wafungwa wa Kipalestina ndani ya magereza ya utawala wa Kizayuni, akisisitiza kuwa tangu kuanza kwa vita vya Gaza, magereza hayo yamegeuka kuwa makaburi ya walio hai.

Allan, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha, aliachiliwa baada ya kutumikia miaka 19 gerezani kupitia makubaliano ya “Tufan al-Ahrar 3”. Alieleza kuwa utawala wa magereza ulianza kutumia mkono wa chuma mara tu baada ya vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza kuanza.

Alifafanua kuwa walinzi wa magereza wamepewa mamlaka ya kiimla, wakipokea amri moja kwa moja kutoka kwa mawaziri wa utawala wa Kizayuni – Ben-Gvir (Waziri wa Usalama wa Ndani) na Smotrich (Waziri wa Fedha).

Kuhusu udhalilishaji wa vitu vitakatifu, Allan alieleza kuwa utawala wa magereza wa Israeli umefanya madhambi makubwa, ikiwemo kutupa nakala za Qur'an ndani ya vyoo, kuzuia adhana, sala za jamaa na za mtu binafsi, na kutishia kuchukua mikeka ya kuswalia.

Kuhusu hali ya maisha gerezani, Allan alisema maji ya moto yamekatwa kabisa katika vyumba vilivyojaa wafungwa 17 hadi 18, na kila mfungwa huruhusiwa kuoga kwa dakika 15 tu kwa siku.

Allan pia alizungumzia sera ya kuwalisha kwa makusudi chakula kidogo, akieleza kuwa mlo mmoja wa sahani mbili za wali na kipande kimoja cha mkate hugawiwa kwa wafungwa 12, hali inayosababisha kupungua kwa uzito kwa nusu na magonjwa makubwa .

Alifichua pia sera ya kuwatengea na kuwatenga wafungwa, ambapo walizuiliwa kutoka nje kwa wiki na miezi kadhaa, na mistari ilichorwa ardhini kuzuia mawasiliano baina yao. Waliokiuka walipigwa na kuadhibiwa vikali.

Allan alisisitiza kuwa yaliyotokea katika magereza ya utawala wa Kizayuni baada ya vita ya Gaza ni jinai ya kimfumo dhidi ya wafungwa wa Kipalestina, na akatoa wito kwa mashirika ya haki za binadamu na ya kibinadamu kuingilia kati haraka.

Tangu Oktoba 7, 2023, utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani na Ulaya umeendeleza mauaji ya halaiki, uharibifu, njaa, uhamishaji wa nguvu, na kuwakamata Wapalestina wa Gaza, huku ukipuuza wito wa kimataifa na maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ya kusitisha vita hiyo.

Mauaji hayo yamesababisha zaidi ya Wapalestina 238,000 kuuawa au kujeruhiwa – wengi wao wakiwa watoto na wanawake – na zaidi ya 11,000 hawajulikani walipo. Maelfu wamekosa makazi, na njaa imewaua wengi, hasa watoto. Miji mingi ya Ukanda wa Gaza imefutwa kabisa.

captcha