IQNA

Hafla ya kufunga Mashindano ya Kitaifa ya Qur'an Iran

21:29 - October 26, 2025
Habari ID: 3481420
IQNA – Hafla ya kufunga awamu ya mwisho ya Mashindano ya 48 ya Kitaifa ya Qur'an ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatarajiwa kufanyika, Oktoba 27, katika mji wa Sanandaj, mkoa wa Kordestan.

Hafla hiyo, ambayo washindi wa makundi mbalimbali watatangazwa na kutunukiwa zawadi, itafanyika siku ya Jumatatu, sambamba na kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bibi Zeynab (SA) na maadhimisho ya Siku ya Wauguzi.

Ukumbi wa Fajr mjini Sanandaj utakuwa mwenyeji wa tukio hilo, ambapo inatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu, Mheshimiwa Seyed Abbas Salehi, pamoja na Mkuu wa Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani, Hujjatul-Islam Seyed Mehdi Khamoushi.

Awamu ya mwisho ya mashindano haya ilianza Oktoba 16 kwa ushiriki wa washiriki 330 wa kiume na wa kike katika makundi 10. Wanaume walishindana katika Ukumbi wa Fajr, huku wanawake wakishiriki katika Ukumbi wa Suleiman Khater wa mji huo.

Katika wiki ya fainali, Kongamano la Kwanza la Kimataifa la “Qur'an ya Negel” lilifanyika Sanandaj, likiwakutanisha maqari wa Kikurdi na wahifadhi wa Qur'an kutoka Iran, Uturuki na Iraq.

Pembeni mwa mashindano haya, mikusanyiko 120 ya Qur'an ilifanyika katika miji mbalimbali ya mkoa wa Kordestan, ikihudhuriwa na makari 30 mashuhuri wa kimataifa. Kwa mujibu wa ripoti, mikusanyiko hiyo ilipokelewa kwa furaha na hadhira ya Mashia na Masunni.

Mashindano haya ya Kitaifa ya Qur'an Tukufu, yanayoandaliwa na Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani, ndiyo mashindano makubwa zaidi ya Qur'an nchini Iran, yakivutia washiriki kutoka maeneo yote ya nchi kushindana katika makundi mbalimbali.

Mashindano haya ya kila mwaka yanachukuliwa kuwa tukio la heshima kubwa katika nyanja ya Qur'an nchini Iran, yakilenga kueneza maadili ya Kiislamu, kukuza maarifa ya Qur'an, na kusherehekea vipaji vya kipekee.

Makundi ya mashindano ni pamoja na: usomaji wa Qur'an, Tarteel, hifadhi ya Qur'an, na Adhana.

/3495154

Habari zinazohusiana
captcha