IQNA

Al-Azhar yalaani shambulio la bomu katika Msikiti wa Jakarta

14:39 - November 08, 2025
Habari ID: 3481486
IQNA – Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri kimelaani mlipuko wa bomu uliotokea katika msikiti mjini Jakarta, mji mkuu wa Indonesia, wakati wa Sala ya Ijumaa, na kujeruhi watu kadhaa.

Ijumaa, bomu liliarifiwa kulipuka ndani ya msikiti ulioko katika Shule ya Upili ya Serikali ya 72 Jakarta, eneo la Kelapa Gading, na kuwaacha watu 54 wakiwa wamejeruhiwa.

Tukio hilo kwa sasa linachunguzwa na vyombo vya usalama kama tendo linaloweza kuwa la kigaidi.

Katika taarifa yake, Al-Azhar ililaani shambulio hilo na kusisitiza kuwa kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia na wanaopenda amani ndani ya nyumba za ibada wakati wakitekeleza ibada za kidini ni uhalifu dhidi ya utu, na ni shambulio wazi kwa maadili yaliyowekwa ili kulinda maisha ya binadamu na kuzuia jamii kuingia katika vurugu na uharibifu.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kitendo hicho ni uthibitisho kwamba wahusika wa uhalifu huu “hawana hata chembe ya mafundisho ya dini, wala thamani za kibinadamu na kimaadili.”

Ikiwaonyesha mshikamano na serikali na wananchi wa Indonesia, Al-Azhar iliomba kwa Mwenyezi Mungu awape walioumia kupona haraka, na alinde watu wa Indonesia na nchi nyingine za Kiislamu dhidi ya madhara na misiba.

Kwa upande mwingine, Kituo cha Al-Azhar cha Kudhibiti Itikadi Kali kimetangaza kwamba kinaufuatilia kwa wasiwasi mkubwa tukio hilo la kusikitisha.

Kituo hicho kilituma salamu za rambirambi na pole kwa Jamhuri ya Indonesia, viongozi wake na wananchi wake, kufuatia mlipuko uliotokea katika Msikiti wa Kelapa Gading ndani ya eneo la elimu wakati wa Sala ya Ijumaa.

Kituo hicho kilisisitiza kuwa matendo kama haya, bila kujali nia au utambulisho wa watenda kosa, hayalingani kabisa na mafundisho yoyote ya dini, uvumilivu, wala misingi ya kibinadamu.

Ingawa picha kutoka eneo la tukio hazionyeshi uharibifu mkubwa wa jengo la msikiti, vikosi vya usalama vya Indonesia vinaendelea na uchunguzi mkali kubaini mazingira na sababu za mlipuko huo.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa mtuhumiwa ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 ambaye kwa sasa anafanyiwa upasuaji, na nia ya shambulio bado inachunguzwa.

3495314

Kishikizo: indonesia msikiti
captcha