IQNA

Papa Leo Kutembelea 'Msikiti wa Sultan Ahmed' Istanbul katika Ziara yake ya Kwanza Kimataifa

16:35 - October 29, 2025
Habari ID: 3481433
IQNA – Kiongozi wa Kanisa Katoliki anapanga kusafiri kuelekea nchini Uturuki, ambapo atatembelea Msikiti wa Sultan Ahmed maarufu kama Blue Mosque, ulioko mjini Istanbul.

Vatikani imetoa ratiba ya ziara ya Papa Leo XIV nchini Lebanon na Uturuki, ambayo itakuwa safari yake ya kwanza rasmi nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican, ziara itaanzia katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara, ambako Papa atakutana na Rais Recep Tayyip Erdogan na kuhutubia viongozi wa serikali, wawakilishi wa jamii, pamoja na wajumbe wa kidiplomasia. Aidha atatembelea Anitkabir na kisha Istanbul. 

Akiwa Istanbul, ratiba yake itajumuisha kikao na maaskofu, makasisi, watawa na watendaji wa kazi za kichungaji katika Kanisa Kuu jijini hapo. Pia atawasalimu wakazi wa kituo cha wazee kinachoendeshwa na kanisa hilo.

Papa ataelekea Iznik—jijulikanalo kihistoria kama Nicaea—kwa helikopta ili kushiriki ibada ya maombi ya kiekumene karibu na mabaki ya kitalu cha kale cha Basilica ya Neophytos. Baada ya hapo atarejea Istanbul kwa kikao binafsi na maaskofu.

Siku inayofuata jijini Istanbul, atatembelea Msikiti wa Sultan Ahmed (Blue Mosque) na kisha kufanya mkutano wa faragha katika Kanisa la Syriac Orthodox la Mor Ephrem na viongozi wa makanisa ya eneo hilo pamoja na jumuiya za Kikristo.

Tarehe 30 Novemba jijini Istanbul, Papa atafanya ziara ya sala katika Kanisa la Armenia, na baadaye kuhudhuria ibada ya Divine Liturgy katika Kanisa la Patriaki, ikifuatiwa na baraka ya kiekumene na mlo wa mchana na Patriaki Bartholomew I.

Sehemu ya ziara jijini Istanbul itafungwa kwa sherehe ya kuagana katika Uwanja wa Ndege wa Ataturk.

Papa atawasili Beirut siku hiyo hiyo, ambako atakutana na uongozi wa kisiasa wa nchi hiyo na kuhutubia viongozi wa serikali, jamii na wanadiplomasia. Ratiba yake Beirut inajumuisha kikao cha faragha na mapatriaki wa Kanisa Katoliki katika Ubalozi wa Vatican, mkusanyiko wa kiekumene na wa kidini katika Uwanja wa Mashahidi, pamoja na hafla na vijana mbele ya Patriaki wa Kimaonite huko Bkerke.

Katika siku zake za mwisho, Papa atasali katika kaburi la  Charbel Makluf huko Annaya, kukutana na viongozi wa dini na watendaji wa kichungaji katika Kituo cha Bikira Maria wa Lebanon huko Harissa, kutembelea wafanyakazi na wagonjwa wa Hospitali ya De La Croix Jal El Dib, kufanya ukimya wa sala katika eneo la mlipuko wa bandari ya Beirut, kisha kuongoza Misa katika Beirut Waterfront, kabla ya sherehe ya kuaga na kurejea Roma.

3495183


captcha