IQNA

Mgombea wa umeya wa Jiji la New York, Mamdani, akabiliana hujuma za chuki dhidi ya dini yake ya Kiislamu

9:31 - October 26, 2025
Habari ID: 3481417
IQNA – Katika kipindi cha kuelekea kuanza kwa upigaji kura wa mapema, mgombea wa umeya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, ametetea imani yake ya Kiislamu huku akilaani “mashambulizi ya kibaguzi na yasiyo na msingi” kutoka kwa wapinzani wake, akionya kuwa chuki hizo dhidi ya Uislamu hazimlengi yeye tu bali pia takribani Waislamu milioni moja wanaoishi jijini humo.

 

Akizungumza kwa hisia kali siku ya Ijumaa, Mamdani alikemea mashambulizi hayo “ya kibaguzi na yasiyo na msingi” siku moja kabla ya kuanza kwa upigaji kura wa mapema katika kinyang’anyiro ambacho anatarajiwa kushinda.

Akihutubia nje ya msikiti ulioko Bronx, Mamdani aliwashutumu wapinzani wake kwa “kuleta chuki hadharani”, akisisitiza kuwa chuki hiyo ya kidini haiathiri yeye pekee kama mgombea wa chama cha Democratic, bali pia Waislamu wapatao milioni moja wanaoishi New York.

“Kuwa Mwislamu New York ni kuzoea kudhalilishwa, lakini kudhalilishwa huko hakutufanyi kuwa tofauti. Wapo Wanewyork wengi wanaokumbana na hali hiyo. Kinachotutofautisha ni namna tunavyokubali au kuvumilia udhalilishaji huo,” alisema Mamdani katika hotuba yake, chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba 4.

Mamdani, ambaye kwa sasa ni mbunge katika Bunge la Jimbo la New York, alisema kuwa ingawa alitaka kampeni yake ijikite kwenye ujumbe wa msingi kuhusu gharama za maisha, wapinzani wake wameonesha wazi kwamba “chuki dhidi ya Uislamu imekuwa eneo pekee wanaloafikiana.”

Hotuba yake ilitolewa siku moja baada ya mpinzani wake mkubwa, gavana wa zamani wa Jimbo la New York Andrew Cuomo, kucheka baada ya mtangazaji wa redio Sid Rosenberg kusema kwamba Mamdani “angefurahia” iwapo shambulio jingine kama la Septemba 11 lingetokea.

Cuomo, ambaye ni mwanachama wa chama cha Democratic lakini alishindwa katika kura za awali za chama hicho Juni iliyopita, alijibu kwa kukubaliana na Rosenberg akisema: “Hilo nalo ni tatizo jingine.”

Basim Elkarra, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya utetezi wa Waislamu, CAIR Action, alieleza matamshi hayo ya Cuomo kuwa “ya kuchukiza, hatari, na yanayomvua sifa za uongozi.”

Akizungumza Ijumaa, Mamdani alisema pia kwamba amekuwa akitukanwa na Curtis Sliwa, mgombea wa chama cha Republican, katika mdahalo wa wagombea alipodai kwamba “Mamdani anaunga mkono jihadi ya kimataifa.” Aliongeza kuwa amekumbana na matangazo kutoka kwa makundi ya kisiasa yenye nguvu (Super PACs) yanayomchora kama “mgaidi au yanayomdhihaki kwa namna anavyokula.”

Alibainisha pia kumbukumbu za “shangazi yake aliyekoma kutumia treni za chini ya ardhi baada ya Septemba 11 kwa sababu hakujisikia salama akiwa amevaa hijabu,” na mfanyakazi wake ambaye “nyumba yake ilipakwa maandishi ya neno terrorist yaani gaidi,” pamoja na ushauri aliowahi kupewa kwamba “asilazimike kuwaambia watu kwamba yeye ni Mwislamu” endapo alitaka kushinda uchaguzi.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na AARP na Gotham Polling and Analytics unaonesha Mamdani anaongoza kwa uungwaji mkono wa asilimia 43.2 ya wapiga kura.

Anayefuata ni Cuomo akiwa na asilimia 28.9, kisha Sliwa na asilimia 19.4, huku 8.4% ya wapiga kura wakibaki bila uamuzi au wakimpenda mgombea mwingine.

Gharama ya maisha imebainishwa kuwa tatizo kuu kwa takriban theluthi mbili ya wapiga kura, huku usalama wa umma na upatikanaji wa makazi nafuu vikitajwa pia kama masuala ya wasiwasi mkubwa.

3495142

captcha