IQNA

Kampeni ya kusambaza nakala 50,000 Qur'ani nchini Mauritania

16:41 - October 29, 2025
Habari ID: 3481434
IQNA – Jumuiya ya Qur'ani Tukufu ya Mauritania imetangaza uzinduzi wa kampeni ya kusambaza nakala 50,000 za Qurani nchini humo.

Tayari usambazaji wa nakala hizo umeanza katika shule kadhaa, misikiti na taasisi za kielimu, kwa mujibu wa taarifa ya Al-Akhbar.

Jumuiya hiyo iliandaa hafla maalumu katika makao makuu yake kuashiria uzinduzi wa kampeni, hafla iliyohudhuriwa na wanazuoni na waqari’ mashuhuri nchini.

Katika hotuba yake, Mohamed el-Amin Ould Cheikhna, Mkurugenzi wa Miongozo ya Kiislamu katika Wizara ya Masuala ya Kiislamu na Elimu ya Jadi ya Mauritania, alieleza kuhusu uhitaji mkubwa wa Misahafu nchini humo.

Alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Dar al-Mushaf (Nyumba ya Msahafu) ambayo ina jukumu la kupitia na kurekebisha nakala za Qur'ani kabla ya kutoa idhini rasmi ya kusambazwa.

Aidha, alitambua mchango wa Jumuiya ya Qur'ani Tukufu ya Mauritania katika kuhakikisha upatikanaji wa nakala za ubora wa juu za Qur'ani kwa kiwango cha kutosha, hatua iliyoondoa kwa kiasi kikubwa upungufu wa misahafu nchini.

Kwa upande wake, Sheikh Sidi Abdelkader Atfail, Mkuu wa Dar al-Mushaf ya Mauritania, alieleza kuhusu ushirikiano uliopo kati ya taasisi yake na Jumuiya ya Qur'ani Tukufu ya Mauritania, na akapongeza juhudi za kusambaza Qur'ani na kuviendeleza vituo vya Qur'ani.

Naye Sayyid al-Hajj, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Qur'ani Tukufu ya Mauritania, alielezea shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo katika kufundisha na kusambaza Qur'ani miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii, jitihada za kueneza elimu ya Qur'ani kwa njia tofauti, pamoja na kuimarisha nafasi ya misikiti na vituo vya Qur'ani katika elimu, malezi na mafunzo ya kijamii.

Al-Hajj alibainisha kuwa hii ni mara ya pili kwa jumuiya kusambaza idadi kubwa ya nakala za Qur'ani katika taasisi, ambapo zoezi la kwanza lilikamilishwa mwaka 2023.

Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania ni nchi ya eneo la Maghreb, Afrika ya Kaskazini Magharibi.

Idadi ya watu inakadiriwa kufikia takribani milioni 4, na karibu wote ni Waislamu.

Shughuli za Qur'ani na programu za kielimu za Kiislamu zinapendwa sana nchini humo. Nchi hii ina historia ndefu ya kuhifadhi Qur'ani, na idadi ya wanawake wahifadhi wa Qur'ani na Hadithi inatajwa kuwa ya kipekee katika ulimwengu wa Kiislamu.

3495186

captcha