IQNA

Washindi wa Mashindano ya Kuhifadhi na Kusoma Qur'an Mauritania wakabidhiwa zawadi

15:42 - October 27, 2025
Habari ID: 3481423
IQNA – Hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa toleo la 12 la mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani Tukufu nchini Mauritania imefanyika katika mji mkuu wa taifa hilo.

Waziri wa utamaduni na sanaa wa Mauritania, Hussein Ould Madou, ndiye aliyewakabidhi washindi zawadi zao.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Idhaa ya Mauritania kwa msaada wa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Ould Cheikh Ghazouani.

Mashindano haya yalikuwa na makundi manne: kuhifadhi Qur'ani yote, kuhifadhi nusu ya Qur'ani, kuhifadhi robo ya Qur'ani, na kundi maalum kwa wanawake ambalo limeongezwa kwa mara ya kwanza mwaka huu.

Katika toleo hili, zawadi za thamani zilitolewa kwa washiriki 63 waliokuwa wamefika hatua ya mwisho kati ya washiriki 1,380 waliokuwa wamejiandikisha.

Majaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walisikiliza usomaji wa washiriki kupitia vituo vya Radio Mauritania vya kitaifa na vya mikoa.

Katika hotuba yake, Waziri Hussein Ould Madou alisema kuwa Rais ameweka kipaumbele katika kueneza maarifa ya Qur'ani Tukufu, uvumilivu, na maadili halisi ya Kiislamu kupitia mikakati ya kitaifa na programu za mageuzi katika nyanja za masuala ya Kiislamu, utamaduni na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa kilichobainisha toleo hili la mashindano makubwa ya Qur'ani ni kuongezwa kwa kundi maalum la wanawake na kutolewa kwa zawadi kwa wasichana waliokamilisha kuhifadhi Qur'ani.

“Hili ni ishara ya kuthamini mchango wa wanawake katika kuhifadhi na kusambaza Qur'an, na ni dhihirisho la dhamira thabiti ya taasisi zetu za kidini na vyombo vya habari kuendeleza maadili ya usawa na ubora kwa wote,” alisisitiza.

Waziri huyo pia alisifu mchango wa Radio Mauritania katika kuimarisha nafasi ya Qur'an Tukufu katika ardhi hiyo, akikumbusha ukubwa wa ujumbe wake katika nyoyo na fikra za watu, na kuimarisha nafasi yake katika maisha ya jamii ya Mauritania ambayo kwa muda mrefu imejulikana kwa uvumilivu, elimu na maarifa.

Alisema kuwa wizara yake imejizatiti kuboresha utendaji wa vyombo vya habari vya umma ili viweze kutekeleza jukumu lao la kuelimisha na kuhabarisha kwa ajili ya dini, taifa na jamii.

Akizungumza pia katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Radio au Idhaa ya Mauritania, Mohamed Abdelkader Ould Allada, alieleza kuwa toleo hili la mashindano limekuwa la kipekee kwa kuongezeka kwa zawadi na ushiriki mpana wa wanawake katika majukumu ya uamuzi na utoaji wa zawadi.

Alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuboresha ubora wa mashindano na kuhamasisha vijana kuhifadhi Qur'ani Tukufu na kuielewa kwa kina.

Aidha, aliongeza kuwa idhaa hiyo inaendelea kuboresha utendaji wake kwa mujibu wa maelekezo ya Rais yanayolenga kuimarisha uwepo wa maadili ya Kiislamu katika taswira ya vyombo vya habari vya kitaifa.

3495156

captcha