IQNA

Mtaalamu: Wazazi Wawaongoze Vijana Katika Mitandao ya Kijamii, Wasijaribu Kuwazuia

13:48 - November 08, 2025
Habari ID: 3481484
IQNA – Mtaalamu wa afya ya akili nchini Iran ameonya kwamba matumizi kupita kiasi ya mitandao ya kijamii yanawafanya vijana kujitenga, huku yakibadilisha maadili yao. Ameitaka jamii ya wazazi Waislamu kuamiliana na watoto kwa huruma, subira na mfano wa vitendo, si kwa kuwabana na kuwadhibiti.

Naser Shafiei, mwanasaikolojia na mtafiti wa tabia za vijana, aliieleza IQNA kwamba wazazi wanapaswa kuacha dhana ya “kumfunza kijana” na kuigeuza kuwa “kuingiliana naye”. Anasema neno “kufundisha” humfanya kijana ajihisi anashambuliwa, ilhali “kuingiliana” humaanisha kusafiri pamoja naye kwa uelewa na mazungumzo.

“Vijana hawapendi kuhubiriwa wala kulaumiwa,” alisema Shafiei. “Imam Ali (a.s.) amesema: ‘Usimlaumu mtu kupita kiasi, kwani lawama za mara kwa mara huzaa chuki na uhasama.’ Ndivyo ilivyo kwa watoto wetu, ukosoaji wa kila wakati unawasukuma watoke nyumbani kimoyo.”

Alisema moja ya sababu kuu zinazowasukuma vijana kuelekea kwa marafiki na jumuiya za mtandaoni kuliko wazazi au wallezi ni hali ya kukubalika bila kuhukumiwa.

“Marafiki zao hawawakosoi — wanasikiliza. Wazazi wanapaswa kujenga hisia hiyo hiyo ya kukubalika ndani ya nyumba.”

“Usipoijua dunia yao, huwezi kuzungumza nao”

Shafiei alisisitiza kuwa mzazi anayetaka mawasiliano yenye mafanikio lazima aielewe dunia anayoishi kijana wake. Bila kufahamu mitandao kama Instagram, alisema, hakuna uelewano wa pamoja, na mazungumzo yanakufa.

Alitaja utafiti kutoka vyuo vya Magharibi unaoonyesha kuwa asilimia 45 ya vijana wanasema wanahisi upweke, licha ya kuishi katika ulimwengu uliojaa mawasiliano.

“Mitandao ya kijamii, licha ya taarifa zisizo na mwisho, inazalisha kizazi kinachojisikia tupu na kimetengwa.”

Kwa sasa, mitandao hiyo ndiyo nguzo mpya ya kuunda utambulisho wa kijana , jukumu ambalo zamani liliongozwa na familia na jamii.

“Wasiposaidiwa, utambulisho wao unaweza kukua nusu nusu, na kuwadhuru wanapokuwa watu wazima.”

“Usipige marufuku lakini simamia”

Aliwaonya wazazi kwamba kusimamia matumizi ya kidijitali hakumaanishi kuzuia.

“Huwezi kuifuta mitandao ya kijamii lakini unaweza kuisimamia. Usimamizi unaanza kwako. Malezi ni kuona, si kusikia , watoto hujifunza kwa wanachoona, si wanachoambiwa.”

Aliwataka wazazi waanze kwa kupunguza matumizi yao wenyewe ya simu.

“Nikiibeba simu yangu kila kona ya nyumba au hata kuingia nayo chumbani, siwezi kumwamuru mwanangu afanye kinyume.”

Athari kiafya na kitabia

Shafiei alionya kwamba matumizi makubwa ya mitandao yanaharibu usingizi wa vijana.

“Usingizi unaposambaratika, mwili na akili hupoteza mizani. Ndipo tunapoona kuwashwa, hasira au tabia zisizo za kawaida.”

Ili kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi , matatizo ambayo yanaongezwa na utegemezi wa kidijitali , alishauri kuwafundisha vijana kuandika mawazo yao.

“Kuandika hupunguza kasi ya wimbi la fikra, na kuzuia zisije kubadilika kuwa vitendo vya msukumo wa kihasira au msukumo wenye madhara.”

Mwisho, aliitaka familia kuimarisha upendo na uhusiano wa kihisia nyumbani, kwa malezi yanayoongozwa na imani na huruma.

“Zungumza na kijana wako kwa uelewa wa zama zake. Ukifanya hivyo, atasikiliza.”

3495309

Kishikizo: jamii vijana dijitali
captcha